Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali imemuagiza Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dkt. Charles Tizeba kukutana na Bodi ya mazao mchanganyiko kwa ajili ya kuliondoa zao la ufuta na kuliingiza katika mfumo wa stakabadhi ghalani.

Ameyasema hayo mapema hii leo wakati akisalimiana na wananchi katika vijiji vya Nangano, Kibutuka na Kiangara alipowasili katika wilaya ya Liwale kwaajili ya ziara ya kikazi ya siku nne mkoani Lindi.

Aidha, Majaliwa amewaagiza wakuu wa mikoa yote inayolima zao la ufuta kukutana na Dkt. Tizeba kwa ajili ya kupanga mfumo mzuri wa uuzaji katika msimu wa mwaka 2016/2017 wakati Serikali ikijipanga kuliingiza zao hilo katika mfumo wa stakabadhi ghalani.

“Tatizo lipo kwenye mfumo wa  uuzaji zao la ufuta, unauzwa kwa bei ya rejareja, wanunuzi wako huru. Serikali imemuagiza Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi kuliondoa zao katika bodi ya mazao mchanganyiko na kuliingiza katika mfumo wa stakabadhi ghalani ili kuboresha bei yake.”amesema Majaliwa

Hata hivyo, Majaliwa ameongeza kuwa Serikali imedhamiria kuondoa tatizo la maji kwa kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama katika umbali usiozidi mita 400.

 

TRA yajibu tetesi za kukagua risiti za mafuta kwa wenye magari barabarani
Mishahara ya wabunge na Rais yapigwa panga Kenya