Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa onyo kali kwa baadhi ya Maafisa Elimu wa Mikoa na Wilaya wanaoshirikiana na walimu kujihusisha na wizi, udanganyifu na uvujaji wa mitihani waache mara moja tabia hiyo na mwenendo huo kwa sababu unalivunjia heshima na hadhi Taifa.

Ametoa onyo hilo jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Sita wa Umoja wa Maafisa Elimu Mikoa na Wilaya (REDEOA), uliofanyika kwenye ukumbi wa chuo cha Mipango kauli mbiu ya mkutano huo inasema “Elimu Bora Itatufikisha Katika Uchumi wa Kati Ifikapo 2025”

Amesema kuwa Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) ni chombo ambacho kwa muda mrefu kimejijengea sifa kubwa sana nchini na barani Afrika, ambapo Serikali imewekeza kiasi kikubwa cha rasilimali ili kukifanya chombo hicho kuwa imara na cha kisasa.

“Kamati za Mitihani za Mikoa na Wilaya ziendelee kusimamia sheria, kanuni na taratibu bila ya woga, upendeleo na tusiyumbishwe na hatua za kinidhamu na kiutumishi kwa mujibu wa sheria, hatua ziendelee kuchukuliwa dhidi ya wote wanaobainika kukiuka sheria, taratibu na miongozo inayotolewa”.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema suala la tatizo la nidhamu mbaya ya wanafunzi ni jukumu la walimu wote, hivyo wanatakiwa watekeleze majukumu yao ya kufundisha, kulea, kuwaongoza na kuwaendeleza wanafunzi kimwili, kiakili na kiroho kwa uadilifu na kuzingatia sheria.

Aidha, amesema kuwa Serikali imesikitishwa sana na matukio ya hivi karibuni ya athari ya viboko kwa wanafunzi shuleni ikiwemo kuvunjwa mikono, kuachwa na makovu pamoja na tukio la kifo cha mwanafunzi Sperius Eradius wa shule ya msingi Kibeta Mkoani Kagera.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi OR-TAMISEMI, Selemani Jafo amewapongeza maafisa Elimu wa Mikoa na Wilaya hao kwa sababu wanafanya kazi kubwa ambayo imechangia kupandisha ufaulu wa kidato cha sita na cha nne nchini, na amewasisitiza kuendelea kufayakazi kwa bidii.

Naye, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amewataka maafisa hao wawe wanatoa taarifa sahihi kuhusu idadi ya wanafunzi kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya kufundishia na kujifunzia.

Awali, Mwenyekiti wa REDEOA, Germana Mung’aho amesema umoja wao unatekeleza majukumu yao ya kusimamia elimu kikamilifu nchini, lengo likiwa ni kumuunga mkono Rais Dkt. John Magufuli, ambaye anasisitiza watu wafanye kazi.

Kadhalika, Mwenyekiti huyo ameiomba Serikali iwapatie magari maafisa hao watakayoyatumia kwa ajili ya kufuatilia maendeleo ya elimu kwenye maeneo yao ya kazi, ambapo Waziri Mkuu amesema suala hilo linashughulikiwa.

Mahakama yafuta kesi ya nyota wa Empire, Jussie Smollet
Jafo ahimiza ushirikiano na WFP