Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka Wakurugenzi wa halmashauri na Maofisa Elimu nchini kutowaondoa katika nyadhifa zao Waratibu wa Elimu Kata na Wakuu wa shule za sekondari wasiokuwa na shahada, walimu wakuu wa shule za msingi wasiokuwa na diploma badala yake wawahamasishe kwenda kusoma.

“Maofisa Elimu na Wakurugenzi msije mkawaondoa wale walimu wakuu kwa zile sifa nilizosema bado muda ukifika tutatangaza.Msije mkawakurupusha sasa hivi waacheni waendelee na kazi zao tutatoa muda ili wajipange viziri,” aliema.

Mwaka huu agosti 20, Waziri Mkuu alisema Waratibu wa Elimu katika ngazi ya Kata na Wakuu wa shule za sekondari wanatakiwa kuwa na shahada huku walimu wakuu kwenye shule wanatakiwa kuwa na diploma.

Alisema Mratibu wa Elimu katika ngazi ya Kata ni lazima awe na shahada ili aweze kutekeleza majukumu yake ya kusimamia utolewaji wa elimu katika shule za sekondari na msingi.

“Wakuu wa shule za sekondari na waratibu wa elimu kata wasiokuwa na shahada wasiondolewe katika nafasi zao kabla ya kupewa nafasi ya kwenda kujiendeleza kwa masomo ili waweze kuwa na vigezo vya kuendelea kushika nyadhifa hizo,” alisema.

Alisema katika kuboresha maslahi ya walimu Serikali imetenga zaidi ya sh. bilioni tano kwa mwezi ambazo ni posho ya madaraka. Waratibu Elimu Kata wanapewa sh 250,000 kwa mwezi huku Wakuu wa shule za sekondari na walimu wakuu katika shule za msingi wanapewa sh. 200,000.

Waziri Mkuu alisema badala ya kuwaondoa kwenye nyadhifa hizo ni vema Wakurugenzi wakawahamasisha walimu hao kwenda kusoma ili na wao wanufaike na posho ya madaraka iliyoanza kutolewa na Serikali hivi karibuni.

 

 

Video: Mazoezi Ya Wazi Ya Jeshi La Polisi Yanatia Hofu - Mbatia
Zitto Kabwe afunguka yake kuhusu Oparesheni UKUTA