Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amewaalika watu wenye itikadi tofauti za kisiasa wasio wa Chama Cha Mapinduzi, kutoficha mawazo yao yanayoweza kuleta maendeleo katika mkoa huo.

Makonda ameyasema hayo leo katika kata ya Majohe wilaya ya Ilala, alipokuwa akizindua ujenzi wa ofisi 402 za walimu mkoani humo uliotokana na kampeni yake maalum ya kuboresha elimu.

Alitoa kauli hiyo, muda mfupi baada ya kumpongeza diwani wa kata hiyo ambaye ni wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo, akimtaka kuendelea na ari yake ya kuonesha ushirikiano katika masuala ya maendeleo bila kujali itikadi za kisiasa.

“Hatujali itikadi ya chama chako. Wewe kama una wazo jema lilete. Watu watakaa watalijadili wataliingiza kwenye utaratibu na tutapata matokeo tunayoyataka,” alisema Makonda.

Aliongeza kuwa maendeleo katika sekta ya elimu yatawafaidisha watanzania wote na hasa watoto ambao baadhi yao hawajui masuala ya vyama vya siasa na itikadi.

Kauli ya Makonda inaunga mkono kauli ya Rais John Magufuli ambaye amekuwa akisisitiza kwenye hotuba zake kuwa ‘maendeleo hayana chama’.

Makonda amesema kuwa mbali na ujenzi wa ofisi hizo ambao umechangiwa na marafiki wa maendeleo kwa kujitolea, rafiki zake wa Marekani pia wameahidi kumpa vifaa vya ofisi hizo.

Alisema kuwa kwa awamu ya kwanza, makontena kumi na mbili yenye vifaa hivyo yataingia bandarini, vivyo hivyo kwa awamu ya pili.

Magazeti ya Tanzania leo Novemba 2, 2017
Thibaut Courtois: Kuishinda Man Utd ni lazima