Hatimaye bondia Floyd Mayweather ametekeleza ahadi aliyowapa mashabiki wake ya kumpiga kwa Knock Out (KO) bingwa wa mapambano ya ngumi na mieleka ya UFC, Conor McGregor katika pambano lililomalizika saa chache zilizopita.

Mayweather amefanikiwa kumzima McGregor katika raundi ya 10 ya pambano hilo baada ya kumuadhibu kwa masumbwi mfululizo bila majibu na kusababisha muamuzi wa pambano hilo kumaliza pambano.

McGregor alifanya vizuri katika raundi nne za kwanza na kuwapa hamasa mashabiki wake lakini mambo yalianza kugeuka kuanzia raundi ya tano ambapo Mayweather alianza kutawala pambano.

Ingawa Mayweather alijaribu kutafuta KO mapema, McGregor alionekana kuwa mgumu na mjanja akikwepa makombora yaliyokuwa yakielekezwa kwake na bingwa huyo ambaye hajawahi kupoteza pambano.

Kutokana na matokeo hayo ya pambano ambalo limevunja rekodi ya mapato ya mapambano yote ya masumbwi, Mayweather ameongeza idadi ya ushindi akiwa na ameshinda mapambano 50 bila kupoteza, na mapambano 27 kwa KO (50-0-27).

Hata hivyo, McGregor ameonesha uwezo mkubwa na kuvunja matarajio ya baadhi ambao walieleza kuwa hatavuka raundi ya 5 kutokana na kutokuwa na uzoefu wowote katika mapambano ya masumbwi akisimama na bingwa wa mapambano hayo.

Majaliwa aishukuru Cuba kwa kuthamini mchango wa mashujaa wa Afrika
Magazeti ya Tanzania leo Agosti 27, 2017