Wakili wa kujitegemea, Leonard Manyama ameingilia kati sakata la kudhulumiwa kiwanja cha mama mjane, Khadija Bakari kilichopo Mbezi Beach jijini Dar es salaam.

Katika sakata hilo, Khadija Bakari ameituhumu familia ya Alex Bura kwa kuvamia kiwanja chake alichoachiwa na marehemu mumewe na kujenga nyumba.

Aidha, Khadija Bakari amesema kuwa amekuwa akipokea vitisho pindi anapodai haki ya kurejeshewa kiwanja chake, kitu ambacho kimemfanya kuomba msaada wa kisheria.

”Kiwanja changu kimevamiwa na huyu Bura, anatumia nguvu ya pesa, sasa mimi mnyonge sina kitu, naombeni sana mnisaidie kupata kiwanja changu, kwani huu ni urithi wa watoto wangu, sina shida na hela ninashida na kiwanja changu, huu ndio urithi wa watoto wangu,”amesema Khadija

Kwa upande wake mlalamikiwa wa kutapeli kiwanja hicho, Alex Bura amesema kuwa kiwanja hicho aliuziwa kihalali na mume wa mama huyo ambaye kwasasa ni marehemu, Norbert Kirti lakini alipotakiwa kuonyesha nyaraka ili kuthibitisha kwamba aliuziwa alishindwa na kusema kuwa walikubaliana kirafiki.

Akizungumzia juu ya sakata hilo baada ya kufika katika eneo la tukio ili kuweza kuona namna ya kutatua mgogoro huo, Mwanasheria wa kujitegemea, Leonard Manyama amesema kuwa ataushughulikia mgogoro huo wa ardhi ili kuhakikisha kila mmoja anapata haki yake.

”Kwakweli kuna mkanganyiko mkubwa sana hapa, lakini mimi kama mwanasheria ni lazima nihakikishe mgogoro huu unamalizika na kila mmoja apate haki yake ya msingi,”amesema Manyama.

 

Marekani yaongeza vikosi Mashariki ya Kati dhidi ya Iran
Video: Fahamu ugonjwa wa ini, dalili na maambukizi