Mwenyekiti wa Bodi ya Parole Taifa, Augustino Lyatonga Mrema amelilalamikia Jeshi la Magereza mkoa wa Dodoma kwa kukwamisha mikakati yake ya kunusuru na kupunguza msongamano wa wafungwa Magerezani ili kuepuka magonjwa ya mlipuko na kusaidia wafungwa wagonjwa, wazee, na wanawake ambao hawajiwezi kutoka Magerezani.

Amesema hayo mapema hii leo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam, Mrema amesema amezuiwa kuendelea na mpango huo bila ya kupewa sababu za msingi na kutanabaisha kuwa kuna wafungwa ambao teyari wamesha lipiwa parole zao na wanatakiwa watoke lakini bado wako gerezani.

“Nilipata wafadhili kama Mchungaji Getrude Lwakatare kajitolea tuwasaidie wale wafungwa waliokosa dhamana tuwasaidie kuwalipia ili watoke magerezani, lakini kuna watu wamejitokeza wanasema eti tunatetea wahalifu hii sio kweli hata kidogo”alisema Mrema.

Aidha, amemuomba Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuliamuru Jeshi la Magereza mkoa wa Dodoma liruhusu zoezi hilo liendelee ili kuisaidia Serikali kuondokana na mzigo mkubwa wa kuhudumia wafungwa wenye makosa madogo madogo na wagonjwa pamoja na wazee.

Mrema ameongeza kuwa kuna watu wanamzunguka ili kukwamisha jithada zake za kuisaidia Serikali na kutoa ombi kwa Waziri Mkuu kuwachukulia hatua kali za kinidhamu viongozi wote wa Jeshi la Magereza Mkoa wa Dodoma wanaokwamisha mpango huo.

 

FIFA Kuzichunguza England, Scotland
Video: Waziri atoa onyo kwa wakuu wa mikoa, ni kuhusu madawati