Marehemu Ruge Mutahaba (Apumzike Kwa Amani), aliwahi kusema kuwa katika dunia ya leo, ‘muogope Mungu na Teknolojia’. Msemo huu umejidhihirisha tena nchini Afrika Kusini, baada ya mpenzi wa msanii maarufu Babes Wodumo kunaswa na teknolojia akimpiga msanii huyo bila kujua kuwa alikuwa anaonekana mubashara kutoka chumbani kwao kupitia ‘Instagram Live’.

Babes Wodumo alionekana akiweka simu yake na kuanza kurusha InstaLive, lakini mpenzi wake anayefahamika kwa jina la Mapmpintsha ambaye pia ni mwanamuziki hakufahamu kuwa dunia ilikuwa inatazama chumbani kwao mubashara muda huo, ndipo alipoanza kumporomoshea makofi mwenzi wake. Babes aliishia kupiga yowe kufuatia kipigo hicho.

Kitendo hicho kimelaaniwa vikali na watu mbambali ambao wameanzisha kampeni iliyokuwa gumzo mtandaoni ya kulaani unyanyasaji wa wanawake #StopWomenAbuse.

Waziri wa Utamaduni wa Afrika Kusini, Nathi Mthethwa ameeleza kusikitishwa na kitendo hicho alichokielezea kuwa ni cha fedheha na kumtaka Babes kumfungulia kesi haraka mpenzi wake ili iwe fundisho kwa wengine.

“Tumechukizwa na vitendo hivi vya mwanamuziki Mapmpintsha, kukamatwa kwenye video akimpiga vibaya mwanamuziki wa kimataifa Babes Wodumo,” ametweet Waziri Mthethwa.

“Hatulaani tu vitendo hivi vya kipuuzi, lakini tunamtaka Babes Wodumo kufungua kesi mara moja dhidi ya huyu Mapmpintsha,” aliongeza.

Dada wa mwimbaji huyo aitwaye Nonduh Simelane aliuambia mtandao wa The Juice kuwa mdogo wake aliumizwa zaidi kisaikolojia lakini amekuwa sawa baada ya kupumzika nyumbani.

Video ya tukio hilo imemuumbua Mapmpintsha kwani mwaka jana alikuwa akituhumiwa kwa kunyanyasa mwimbaji huyo lakini alikana kuwa hajawahi kumgusa.

Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Machi 5, 2019
Magufuli awashangaa Polisi kutekwa Mo Dewji, ‘Watanzania sio wajinga’