Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda amesema kuwa amefurahi kupokea heshima ya kuwa mlezi wa Mradi wa Utambuzi wa Sanaa za Ufundi Tanzania (TACIP), ambapo ameahidi kuwa asimama kidete kuhakikisha kuwa mradi huo unafanikiwa na kuwakomboa wasanii kama ulivyolengwa.

Pinda amesema kuwa tasnia ya sanaa ina nafasi kubwa ya kuweza kuondoa umaskini katika ngazi zote kama itatumiwa vizuri.

Amesema hayo nyumbani kwake Nzinje, nje kidogo ya Jiji la Dodoma, wakati alipokutana na wawakilishi wa TACIP waliokwenda kumuomba awe mlezi (champion) wa mradi huo.

“Tasnia ya sanaa ni nafasi kubwa ya ajabu ya kuondoa umaskini katika ngazi zote kama tutaitumia vizuri. Nimepokea heshima hii ya kuwa mlezi wa TACIP na naahidi kuwa sitawaangusha,” alisema.

Pinda amesema kuwa alipata bahati ya kukutana na viongozi wa Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) jijini Dodoma hivi karibuni na alichobaini ni kwamba katika kila eneo walilojadili, walikuwa wakihusisha na suala la sanaa na utamaduni na jinsi inavyoweza kutumika kama njia ya kutoa suluhisho ya tatizo liliopo.

“Wenzetu wako makini sana na kutunza utamaduni wao, lolote atakalojadili lazima aweke umuhimu wa sanaa na utamaduni wao. Wenzetu wameona utamduni ni zana ya kutatua tatizo lolote linaloizunguka jamii yao,” alisema.

Amesema anatamani wasanii wa Tanzania wabaini ni mambo gani wanaweza kujifunza kutoka kwa Wachina katika kukuza sanaa, kwani katika kukabiliana na tatizo la mazingira, wametumia wasanii kupeleka ujumbe wa kuelezea maovu dhidi ya mazingira na mambo mazuri yanayodumisha mazingira, pia katika elimu wametumia sanaa.

“Huku kwetu wasanii wanatumika kutoa burudani, inabidi tubadilishe mtazamo huu kwa kushirikiana na Serikali kupeleka ujumbe huu mpya,” amesema.

Aidha, amekiri kuwa tasnia ya sanaa ina washiriki zaidi ya milioni sita ambao hawajawahi kuunganishwa na chombo maalum na kwamba kuanzishwa kwa TACIP kutaleta ukombozi kwenye sekta hiyo muhimu kwa Taifa.

Mapema, Mratibu wa mradi huo, Macmillan George amemweleza Pinda kwamba mradi umepangwa kutekelezwa kwenye kanda sita ambazo ni Pwani Mashariki, Nyanda za Juu Kusini, Kaskazini na Magharibi. Nyingine ni kanda ya Kati na kanda ya Ziwa.

Amesema wiki ijayo wanatarajia kuanza kukusanya taarifa za wasanii wa sanaa za ufundi kwa kuanza na mkoa wa Dar es Salaam. Wasanii hao wanajumuisha wachoraji, wachongaji (sculptors), wanasanaa za mikono (crafts), wanasanaa jumuishi (peripheral artists), wafinyanzi (ceramics) na wabunifu (designers).

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nicholaus William ambaye aliambatana na viongozi hao, amesema kuwa Serikali inaubeba mradi huo kwa uzito mkubwa, kwani kuwepo kwa mradi huo kunatarajiwa kutatua changamoto za wasanii nchini ambazo zimedumu kwa muda mrefu.

Kaulimbiu ya mradi huo ni: “Jitambue, Tambulika, Inalipa.”

Mradi wa TACIP (Tanzania Arts and Crafts Identification Project) unatekelezwa kwa ubia kati ya TAFCA (Tanzania Arts and Crafts Identification Project) na Kampuni ya kizawa ya DataVision International na umelenga kuiwezesha sekta ya sanaa za ufundi Tanzania Bara kuwaongezea kipato washiriki wake, hususan katika kujikwamua kutoka kwenye balaa la umasikini na kuwawezesha kuchangia pato la Taifa.

Aidha, Mradi wa TACIP umelenga kuwatambua washiriki wa sekta hiyo na kuwapatia vitambulisho vya kisasa vya kieletroniki, kuanzisha tovuti maalumu ya wasanii hao yenye taarifa za majina, jinsi, umri, mahali walipo na wanachozalisha, kufungua tovuti ya ‘e-commerce portal’ ili kuwezesha biashara mtandao ya kazi za sanaa za ufundi, kuwahamasisha wajisajili kisheria na kujiunga katika vikundi na vyama ili wawe na nguvu ya sauti na waweze kukubalika kukopa katika taasisi za fedha.

Video: Hii Ndiyo Dawa ya Mdudu Anayeitafuna Sanaa Tanzania

Video: Maajabu ya Masanja msanii anayechora kwa kutumia moto, aitaja TACIP mkombozi wa wasanii

IGP Sirro afanya mabadiliko kwa baadhi ya makamanda wa polisi
Video: Ridhiwani afunguka anavyoutamani ukatibu Mkuu CCM

Comments

comments