Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, limewakamata watuhumiwa wawili pamoja na bunduki iliyotengeneza kienyeji waliyokuwa wakiitumia kufanyia matukio ya ujambazi.

Akiongea leo na Waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi wa kanda hiyo, Simon Sirro amesema kuwa watuhumiwa hao walikutwa na bunduki hiyo iliyotengenezwa kienyeji kwa muundo wa ‘short gun’ pamoja na risasi moja.

Kamanda Sirro alisema kuwa watuhumiwa hao walikamatwa Jumatano wiki hii katika eneo la Sinza Kangaroo jijini humo. Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Gaiton Mulika (18) na Mbelwa Tumweibesi (27), ambaye ni mkazi wa Mbezi Makonde.

Aidha, alisema kuwa watuhumiwa hao walitaja matukio mbalimbali waliyotekeleza kwa kutumia silaha hiyo na kwamba bado hawajafikishwa mahakamani kwakuwa wanaendelea kuwataja watu waliokuwa wanashirikiana nao.

Katika hatua nyingine, Kamanda Sirro alisema kuwa Jeshi hilo limefanikiwa kwa kiasi kikubwa kukamata genge la kiharifu linalojiita ‘Panya Road’, ambapo 53 walitiwa mbaroni hivi karibuni.

“Tumekuwa na mafanikio makubwa sana. Kukamatwakwa genge la vijana wa Panya Roads 53, na tunaendelea na oparesheni mbalimbali za kuwakamata hawa panya roads,” alisema Kamanda Sirro. Alisema watu hao walikamatwa katika eneo la Kinyerezi, Tabata-Mawenzi.

Kamanda Sirro aliwaomba wananchi kuendelea kutoa taarifa kwa jeshi hilo zitakazofanikisha kuwakamata Panya Roads, na wazazi kuhakikisha wanawakanya watoto wao kwani genge hilo linaundwa na vijana wadogo.

Ufaulu Washuka Kidato cha Sita, Arusha,Dar na Pwani zang'ara 10 Bora
Matokeo ya Ualimu (DSEE) na GATCE 2016