Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli na mkewe, mama Janeth Magufuli leo wamemtembelea Mama Maria Nyerere nyumbani kwake Msasani jijini Dar es salaam baada yakuhudhuria Misa Maalumu kumuombea Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere iliyofanyika katika Kanisa la Mtakatifu Petro Oysterbay jijini Dar es salaam leo Jumapili Oktoba 14, 2018.

Wakati akizungumza na Mama Maria Nyerere, Rais Magufuli amesema Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea kumuenzi Baba wa Taifa Hayati Mwlalimu Julius Kambarage Nyerere kwa kuhakikisha fikra na mipango mizuri aliyoiweka inatekelezwa kwa manufaa ya Watanzania wote.

Amesema kuwa kuwa Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alifanya kazi kubwa ya kujenga misingi imara ya nchi kuwa na amani, umoja na mshikamano na pia kujenga misingi ya uchumi wa kujitegemea kupitia Azimio la Arusha.

Naye, Mama Maria Nyerere amemshukuru Rais Magufuli kwa kuendelea kumuenzi Baba wa Taifa na amemhakikishia kuwa yeye na wanamaombi wenzake pamoja na Watanzania wote wanamuombea heri yeye, viongozi wote na Taifa kwa ujumla.

Awali, leo asubuhi Rais Magufuli aliungana na Waumini wa Kanisa la Mtakatifu Petro, Oysterbay Jijini Dar es Salaam, pamoja na watanzania wote kusali Misa Takatifu ambapo Waumini hao wamemuombea Baba wa Taifa, aliyefariki dunia tarehe 14 Oktoba, 1999.

JPM anena kuhusu kuhamia Dodoma
Msako wa waliomteka Mo Dewji washika Bahari ya Hindi