Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete amesema kuwa moja kati ya ndoto zake ni kushika nafasi za ukatibu mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), nafasi ambayo hivi sasa inashikiliwa na Dkt. Bashiru Ally.

Ridhiwani ambaye ni mtoto wa Rais mstaafu, Dkt. Jakaya Kikwete ameyasema hayo hivi karibuni alipofanya mahojiano maalum na Dar24 bungeni jijini Dodoma.

“Siku zote mimi natamani kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi. Ni kazi ambayo nina passion (shauku) nayo,” Ridhiwani aliiambia Dar24 na kuongeza, “Chama cha Mapinduzi nikipewa mimi ukatibu mkuu wake kitakuwa salama sana.”

Alisema kuwa anaamini kuwa anaweza kufanya kazi hiyo vizuri muda utakapofika kama atapewa nafasi ya kuendeleza kazi nzuri iliyofanywa na viongozi waliotangulia kwa sababu chama hicho kimekuwa sehemu ya maisha yake tangu akiwa mdogo.

“Mimi nimeanzia kwenye chipukizi. Sijakurupuka tu nimetoka shule nimefaulu nimekosa kazi niamue kuingia kwenye chama, hapana,” alisema.

Mbunge huyo ameeleza kuwa tangu akiwa na umri wa miaka mitano alikuwa tayari ameanza kufanya kazi za chama hicho kama chipukizi; na amekumbuka mwaka 1984 katika sherehe za kumbukumbu ya kuzaliwa chama hicho zilizofanyika Bagamoyo kuwa ni yeye ndiye aliyeongoza gwaride la chipukizi.

Amesema kuwa kutokana na kuishi akiwa ndani ya chama hicho amekuwa na uzoefu mkubwa na kwamba kuna wakati anaona kuna sehemu ya kufanyia marekebisho.

“Nina mapenzi na chama changu na napenda kuwa kiongozi wa chama hiki na naamini kuwa hii ndiyo nafasi ambayo nikipewa ninaweza kukifanya chama hiki na kikaendelea kuwa na nguvu zaidi katika Afrika,” Ridhiwani aliiambia Dar24 na kusisitiza kuwa hajawahi kutamani kuwa Rais kutokana na namna alivyoona mchakato wa nafasi hiyo kwa baba yake.

Kwa mujibu wa Katiba ya CCM, Katibu Mkuu Taifa huteuliwa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama hicho katika kikao kinachoongozwa na Mwenyekiti wake ngazi ya taifa.

Video: Pinda aupa tano mradi wa TACIP, 'Utaleta ukombozi kwenye sekta muhimu'
TRA yakanusha 'Whatsapp' kuanza kulipiwa kodi

Comments

comments