Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete (CCM) ametoa mtazamo wake kuhusu hali ya kisiasa nchini na kile kitakachoweza kutokea kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2020, hususan hali ya upinzani.

Akizungumza kwenye mahojiano maalum na Dar24 yaliyofanyika Msoga, Ridhiwani alisema kuwa licha ya kile kinachoendelea, anaamini bado wapinzani wanaweza kuibua upinzani kwenye uchaguzi huo kutokana na namna ambavyo wapinzani wataamua kuyachukulia yaliyofanyika hata kama ni mazuri.

“Unaweza ukategemea kusiwe na upinzani thabiti, lakini akatokea mtu akasema ‘eeh bana eeh, huyu jamaa kafanya kila kitu anachokita sasa imefika muda wake aondoke na sisi wengine tuingie tufanye yale ambayo wananchi wanayataka’,” alisema.

“Kwahiyo upinzani thabiti unategemea na hali ya watu watakaokuwepo kipindi hicho na jinsi wanavyobeba ajenda zao. Kwa sababu ajenda za maisha haziishi,” aliongeza.

Alisisitiza kuwa kutokuwepo kwa upinzani thabiti au la ni suala linalotegemea wakati husika.

Mbunge huyo ambaye ni mtoto wa Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete alitolea mfano wa hospitali iliyojengwa Msoga kuwa anaweza akatokea mtu pamoja na ujenzi huo akaamua kuonesha kutoridhishwa na baadhi ya mambo na hiyo ndiyo ikawa ajenda yake kwenye uchaguzi.

Katika hatua nyingine, Ridhiwani aliwashauri wapinzani kujaribu kukubaliana na mambo mazuri yanayofanywa na Serikali na kuunga mkono badala ya kuamua kupinga tu.

“Kama mtu anafanya vizuri mnakaa mnasema ‘fulani amefanya vizuri na sisi tumuunge mkono. Isije kufika muda nyie kazi yenu ikawa ni kupinga tu… yaani ikifika wakati wa uchaguzi mnaanza tu ‘huyu hafai!’ Na ukiuliza hafai kwa nini unaambiwa hafai tu,” alisema.

Mtunga sheria huyo alisema kuwa hafurahishwi na hamahama ya vyama inayoendelea lakini kwakuwa ni jambo linaloruhusiwa kikatiba na sababu zinazotolewa zina mashiko basi hakuna ubaya.

Mama yake Osama anena kwa mara ya kwanza kuhusu mwanaye
Video: Kauli ya JPM yamvuruga RC Makonda, Mkurugenzi Twaweza aibuliwa zengwe la uraia