Ukumbi wa mkutano wa Kamati ya Akaunti nchini Kenya jana uligeuka kwa muda kuwa ulingo wa ndondi wa mchangani baada ya Seneta wa Nairobi, Mike Sonko na Gavana wa Jiji hilo, Evans Kidero kukamatana mashati.

Tukio hilo lililorekodiwa na waandishi wa habari jana asubuhi katika kikao cha Kamati ya Mambo ya Fedha baada ya Sonko kumtuhumu Gavana Kidero kwa kufanya ubadhirifu wa mali za umma kwa kuzigeuza kuwa mali zake na mkewe huku akieleza kuwa na nyaraka zinazoonesha ushahidi wa mambo.

Seneta Sonko aliendelea kumshambulia Gavana huyo aliyekuwa kimya kiasi hadi ulipofika wakati wa muda wa mapumziko ambapo aliendelea kumrushia maneno akionesha kukerwa na alichokifanya. Ndipo uvumilivu ulipomshinda Gavana huyo na kujibu mapigo kwa vitendo.

Ugomvi kati ya wawili hao ulianza ghafla kabla ya viongozi wengine waliohudhuria kujaribu kuzima moto ambao hata hivyo ulikuwa mgumu kuzimika hadi walinzi wa Seneta Sonko na Gavana Kidero kuingilia kati kuwasaidia maboss wao kutoendelea kuvutana.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Profesa Anyang’ Nyong’o amemtaka Gavana Kidero kuwasilisha ushahidi wake kutokana na mashaka yaliyoonekana kwenye ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali wa nchi hiyo, hususan kueleza kiasi kilichokusanywa na serikali katika kodi ya ardhi jijini humo.

Maalim Seif afunguka kuhusu uamuzi wa Lipumba, akana nukuu iliyosambazwa
Rais Magufuli amemteua Prof. Rubaratuka kuwa Mwenyekiti TPA