Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Faustine Ndugulile amesema kuwa wagonjwa wanaokwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) bila kufuata taratibu za rufaa ndio chanzo cha kuongezeka kwa gharama za vipimo.

Dkt. Ndugulile amesema hayo leo Septemba 13, 2019 Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Mariam Kisangi akihoji kwanini wananchi wanatozwa gharama kubwa mara mbili wanapokwenda kuomba huduma za vipimo katika hospitali hiyo ya Taifa.

Dkt. Ndugulile amebainisha kuwa utaratibu wa kupata huduma katika hospitali lazima ufuatwe kwani mgonjwa ambaye hajapitia hatua hizo hutozwa gharama kubwa kwasababu anahesabika kama mgonjwa binafsi.

“Wagonjwa wote ambao wanapitia taratibu za rufaa kuanzia ngazi ya zahanati huwa wanahudumiwa vipimo hivyo kwa gharama ndogo lakini mgonjwa ambaye hajapitia hatua hizo hutozwa gharama kubwa kwani anahesabika kama mgonjwa binafsi,” amesema Dkt. Ndugulile

Awali, katika swali la msingi, Mbunge huyo alitaka kujua Serikali ina mkakati gani kupeleka mashine za kufulia katika hospitali za Rufaa Amana, Mwananyamala na Temeke ambazo hazina mashine hizo.

Akijibu swali hilo, ameeleza kuwa taratibu za kununua mashine zinaendelea kwani Amana imeshatenga eneo kwa ajili kujenga chumba cha utakatishaji huku wakiwa kwenye mchakato wa kununua mashine kubwa ya Sh 80 milioni.

Mbunge ataka sheria kuwabana wanaotoa ushuzi ndani ya ndege
Tanzania: Wanawake, wanaume 50/50 kufikia 2030