Simba SC imeingia hatua ya mwisho ya mchujo wa kuwania kushiriki hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya wenyeji, Mbabane Swallows katika Uwanja wa Mavuso mjini Manzini, Eswatini, zamani Swaziland.
 
Simba SC inasonga mbele kwa ushindi wa jumla wa mabao 8-1, baada ya kushinda 4-1 kwenye mchezo wa kwanza wa Raundi ya Awali ya mchujo Jumatano ya wiki iliyopita Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
 
Katika mchezo uliochezeshwa na refa, Nelson Emile Fred aliyesaidiwa na washika vibendera Hensley Danny Petrousse na Gerard Pool, wote wa Shelisheli, hadi mapumziko Simba SC walikuwa mbele kwa mabao 2-0.
 
Aidha, magoli hayo yaliyopatikana kipindi cha kwanza yalifungwa na kiungo Mzambia, Clatous Chama dakika ya 28 na 33 na kipindi cha pili wachezaji wengine wawili wa kigeni Mganda Emmanuel Okwi na Mnyarwanda Meddie Kagere wakaunenepesha ushindi wa Simba.
 
Okwi alifunga dakika ya 52 na Kagere aliye katika msimu wake wa kwanza tu tangu asajliwe Simba SC akitokea Gor Mahia ya Kenya akafunga dakika ya 63.
 
  • Masau Bwire ajipa faraja baada ya kichapo cha Azam FC
  • Waziri Mwakyembe aitaka Taifa Stars kutowaangusha Watanzania
  • Video: BMT yatuma salamu kwa wenyeviti wa riadha wa mikoa
 
Simba SC sasa itakutana na mshindi wa jumla wa mchezo kati ya UD Songo ya Msumbiji na Nkana FC ya Zambia zinazorudiana leo Uwanja wa Nkana mjini Kitwe.
 
Mchezo wa kwanza, Nkana FC timu anayochezea beki wa zamani wa Simba SC na Yanga SC za Dar es Salaam, Hassan Kessy ilishinda 2-1 ugenini Uwanja wa Chiveve mjini Beira.

Video: Mawaziri washirika wa Membe kitanzini, Sakata la mafao hoja binafsi kutua Bungeni
Makamba afunguka sakata la Membe, akumbushia ya TANU