Kamishna wa Kanda Maalumu ya Dar es salaam, Simon Sirro amesema kuwa watuhumiwa wote wa dawa za kulevya ambao hawajaripoti wanatakiwa wajisalimishe wenyewe kuliko kusubiri kutumika kwa nguvu kubwa Jeshi la Polisi.

Ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari mapema hii leo jijini Dar es salaam, amesema kuwa watu hao wanatakiwa kujisalimisha ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.

Amesema idadi kubwa ya watumiaji wa dawa hizo za kulevya imepungua kwa kiasi kikubwa hivyo amewaomba wananchi wa Jiji la Dar es salaam kushirikiana na Jeshi la Polisi ili kuweza kuwabaini kwa wale waliobaki.

“Hakuna sababu ya kusubiri nguvu itumike kutoka Jeshi la Polisi kwani tukiamua kufanya hivyo, watalaumu bure Jeshi letu, hivyo waje wajisalimishe wenyewe,”amesema Sirro.

Aidha, katika hatua nyingine Sirro amewatahadharisha wananchi wa Jiji la Dar es salaam kuwa makini na matapeli ambao wanawarubuni wananchi kuwatafutia nafasi za kazi katika makampuni mbalimbali kwa masharti ya kuwapatia fedha.

Hata hivyo, amewataka kupuuza taarifa zozote wanazopata kutoka kwa watu wasiowajua kwani wengi ni matapeli ambao wanatumia njia hiyo kwaajili ya kujipatia kipato.

Facebook, Instagram waanzisha program kuwashughulikia wanaosambaza picha za utupu
Viongozi wa makampuni 50 Israel kuwasili Tanzania