Mbunge wa Mbeya Mjini kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Joseph ‘Sugu’ Mbilinyi amemhakikishia Rais John Magufuli kuwa anamuunga mkono kwa kazi anayoifanya lakini anafanya hivyo bila kuhama chama chake.

Akizungumza leo katika mkutano wa Rais Magufuli jijini Mbeya, Sugu amemuomba kupuuzia taarifa kuwa hawampendi na hawamuungi mkono, akieleza kuwa wanamuunga mkono kwa mambo mengi na kukosoa machache lakini wanaamini hapewi taarifa kamili.

Aidha, Mbunge huyo ambaye alikuwa mmoja kati ya waliompokea Rais Magufuli akitokea nchini Malawi, alimueleza mkuu huyo wa nchi kuwa yeye ni mfuasi wake wa falsafa ya ‘maendeleo hayana vyama’; na akamuomba amruhusu kumpa kazi ya kuwa njia ya kuendesha mazungumzo ya kuondoa tofauti za kisiasa kwenye masuala ya maendeleo katika jiji hilo na hata katika ngazi ya Taifa.

“Kwa unyenyekevu hata ukiangalia, tulivyokaa hapa unaona kabisa kuna mgawanyiko, watu wetu wa Chadema wako hapa… wako kule nyuma, hebu nyoosheni mikono…Wamekuja huku wamewabana, na wewe unasema haufuati vyama; na mimi nimekushika, ninakufuata na ni mmoja kati ya wanaokuunga mkono bila kuhama chama na nitaendelea kukuunga mkono hadi mwisho,” alisema mbunge huyo.

“Kwahiyo mimi kwakuwa ni rafiki yako na ni kijana wako wasikwambie ‘mara matusi, au hatukupendi, sio kweli. Jana kuna Mwenyekiti wangu alikamatwa kwa madai eti anapanga kufanya fujo kwenye mkutano wa Rais, haiwezekani, hicho kitu hakiwezekani. Nakuomba sana Mheshimiwa Rais, mimi kijana wako kama itakupendeza niwe channel ya dialogue ili kuondoa haya mafundofundo hapa Mbeya hata kitaifa ikiwezekana,” aliongeza.

Akizungumza katika mkutano huo, Rais Magufuli alieleza kuwa yeye ni Rais wa wote akisisitiza kuwa anaamini maendeleo hayana chama, hivyo akampongeza Sugu kwa kumpokea uwanja wa ndege na kushiriki katika ziara yake.

“Hata mbunge wa hapa ndugu Sugu sijui ndio jina lake halisi, alisugua mpaka airport akanisindikiza mpaka nilipoenda, nikadhani labda hii ndio njia ya kuanza kuelekea CCM, lakini yote kwa yote huo ndio umoja wa Utanzania,” alisema Rais Magufuli.

Aliyemshtaki R Kelly kwa makosa ya kingono ashinda kesi
CCM Njombe yawataka Watanzania kuulinda na kuimarisha Muungano

Comments

comments