Bingwa wa Dunia wa Masumbwi ya Uzito wa Juu, Anthony Joshua (A.J) amesukumwa kwa hasira na mpinzani wake, Jarrell Miller kwa sababu ya tabasamu lake walipokutana.

Miller ambaye alizua tafrani katika mkutano wao na waandishi wa habari jijini New York nchini Marekani, amesema kuwa alijikuta akimsukuma A.J kwa kuwa alitabasamu kwa dharau walipokutana.

A.J ambaye alikuwa ameweka mikono yake miwili nyuma, alirejea akimuita tena Miller, lakini wakati huu walinzi waliamka na kuhakikisha hakuna anayemgusa mwenzake licha wawili hao kujaribu tena kukamatana.

Wababe hao ambao wote hawajawahi kupigwa, wanatarajia kupambana ulingoni Juni Mosi mwaka huu jijini humo.

“Aliniudhi sana, alikuwa anatabasamu… hakukuwa na kitu cha kumfanya atabasamu pale. Nimekuwa nikimuwaza Anthony Joshua kila wakati. Nikilala ni ‘Anthony Joshua’, nikiamka ‘Anthony Joshua’, nawaza nitakavyompasua,” alisema Miller.

“Katika mkutano uliopita aliniita akaniambia anataka tuzungumze. Mimi sina kitu cha kuongea na mtu sasa hivi. Kama unataka tuongee njoo unipige konde usoni, hayo ndio mazungumzo yetu, ninaheshimu vita,” aliongeza.

Kwa upande wake A.J alieleza kuwa alitaka kumtunzia heshima Miller lakini ameona amchakaze tu. Alidai kuwa Miller hana uwezo wa kupambana naye kwakuwa ameshawahi kupigwa chini mara saba [na Tyson Fury].

“Hawezi kupiga konde la maana. Ni bondia mrahisi zaidi katika ngumi za uzito wa juu. Hajawahi kufanya chochote cha maana wakati wa ngumi za ridhaa na wakati wa ngumi za kulipwa,” alisema A.J.

“Juni 1 atakutana na bingwa wa kweli, ni wazi kuwa nitamnyanyasa na kumpiga kwa KO, huo ndio ukweli,” aliongeza.

Miller hakuwa chaguo la kwanza la A.J, alikuwa akiwataka Deontay Wilder au Tyson Fury lakini amewakosa kwani mabondia hao wamejikita katika kuhakikisha wanapanda tena ulingoni kwa ajili ya pambano lao la marudiano baada ya kutoka sare katika pambano la kwanza.

Mbunge wa Mafinga akabidhi Magari mawili Idara ya Elimu
Serikali yakerwa na vitendo vya mauaji na unyang'anyi mipakani