Waziri wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema kuwa wazazi wana jukumu la kulea watoto kwenye misingi ya kumcha Mungu ili Taifa liweze kuwa na watu waadilifu na wachapakazi.

“Taifa la watu waadilifu na wachapakazi huanzia katika ngazi ya familia. Kama kaya zetu haziishi kwa uadilifu, ni vigumu sana kuwa na Taifa lenye wananchi waadilifu. Ni muhimu basi familia zetu zihakikishe kuwa tunakuwa na watoto wenye hofu ya Mungu na wenye kumcha Mungu,” alisema.

Majaliwa amesema hayo wakati akizungumza na wageni waliohudhuria harambee ya kuchangia ujenzi wa kanisa na nyumba ya Paroko katika Parokia Teule ya Zuzu, nje kidogo ya mji wa Dodoma.

Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda alisema harambee hiyo inafuatia uamuzi wa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dodoma, Mhashamu Beatus Kinyaiya wa kuiteua Zuzu iwe parokia.

“Sasa hivi tulikuwa na kigango. Kuteuliwa kuwa parokia maana yake tutakuwa na padre anakaa hapa Zuzu saa 24 na tutakuwa na ibada kila Jumapili, na katikati ya wiki kadri ratiba zitakavyoruhusu.

“Kikubwa tunachopaswa kufanya kufuatia uamuzi huo, ni kuhakikisha kuwa mapadre wana nyumba ya kuishi. Sasa hivi, wa kwetu anakaa Dodoma mjini. Kwa hiyo tuna kazi ya kukarabati kanisa, lakini kwanza tukamilishe ujenzi wa nyumba ya mapadri,” alisema wakati akielezea madhumuni ya harambee hiyo.

 

Ole Sendeka Ampongeza Lowassa, Amshukuru
Majaliwa ashiriki mazishi ya mara ya pili ya baba mzazi wa Spika Ndugai