Usiku wa kuamkia leo ulikuwa usiku wa kukata ngebe kwenye ulimwengu wa masumbwi baada ya bondia Terrence ‘The Bud’ Crawford ‘kumfunza adabu’ aliyekuwa bingwa wa dunia wa masumbwi uzito wa Welterweight, Jeff Horn kutoka Australia.

Likiwa pambano lake la kwanza nchini Marekani, Horn aliyekuwa anashikilia mkanda wa ubingwa aliouchukua kutoka kwa nguli Manny Pacquiao mwaka jana nchini kwao Australia, alijikuta akipigwa kila raundi na kuzimishwa katika raundi ya tisa (9).

Crawford ambaye anatajwa kuwa katika nafasi ya pili ya mabondia bora zaidi duniani kwa sasa baada ya Vasyl Lomanchenko, alitawala pambano hilo akishinda kila raundi na kumtesa Horn kabla ya mwamuzi kusimamisha pambano.

“Ni bondia mzuri. Nilidhani nitampiga akiwa anakuja mbele, na nilianza kujaribu sana. Kazi nzuri, Terrence Crawford, bondia bora. Alikuwa na nguvu na hakuonekana kama ni mwenye mwili mdogo. Huo ni ukweli,” alisema Horn (18-1-1, 12 KOs) akikubali matokeo.

Jana ilikuwa mara ya kwanza kwa Horn ambaye pia ni mwalimu wa shule ya awali kupoteza pambano, lakini ilikuwa mbaya zaidi kwakuwa alipoteza kila raundi ya mchezo.

Crawford (33-0, 24 KOs) ambaye ameweka rekodi ya kutowahi kupoteza pambano, amemtaka promota Bob Arum kuandaa pambano kati yake na wababe wengine wanaotajwa kuwa moto kama Eroll Spence, Lomachenko na Mikey Gacia.

Ndoto ya Simba kwenda Uingereza yaota mbawa
Wanachama Yanga wapinga kujiuzulu kwa Manji