Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema Serikali itawashughulikia watu wote  wanaotoa matamshi ya kichochezi nchini bila ya kujali nyadhifa zao.

Majaliwa amesema hayo wakati wa ibada ya mazishi ya mke wa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe, Linnah Mwakyembe iliyofanyika wilayani Kyela, amesema ni vema watu wakawa makini na kijiepusha kutoa matamshi ambayo yataathiri mfumo wa maisha kwa wananchi wengine.

Amesema Serikali haitavumilia kuona baadhi ya watu wakitoa matamshi ambayo hayana tija kwa jamii na badala yake yanalenga kuwavuruga wananchi na kuchochea migogoro.

“Tutashughulika na watu wote wanaotoa matamshi ya kichochezi, popote walipo bila ya kujali uwezo wao, vyeo vyao na mamlaka walizonazo.”

Majaliwa pia amewaomba viongozi wa dini waendelee kuliombea Taifa na viongozi wake na kwamba Serikali inawategemea na iko pamoja nao.  Kauli hiyo ni baada ya Askofu wa Kanisa la Evarinjerical Brother Hood, Rabison Mwakanani kuonya vitendo vya baadhi ya watu kumtukana Rais Dkt. John Magufuli.

“Rais Dkt. Magufuli amefanya mambo mengi makubwa kwa ajili ya maendeleo. Wanaofanya hivyo wasidhani kama wanamtukana Rais tu bali wanawatukana Watanzania wote waliomchagua wakiwemo viongozi wa dini.”

Aidha, Majaliwa amewaomba wananchi wote washirikiane kwa pamoja kumuombea Dkt. Mwakyembe na familia yake ili Mwenyezi Mungu aweze kuwafariji katika kipindi hiki kigumu.

“Wajibu wetu sote ni kumuomba Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema. Tunajua kwa sasa Dkt. Mwakyembe yuko katika wakati mgumu, namuhakikishia kwamba hayuko peke yake kwani Serikali iko pamoja naye katika kipindi hiki kigumu.”

 

Video: TCU yatii agizo la JPM, yatangaza rasmi taratibu za kujiunga na vyuo vikuu
Video: Watoto 3 walionusurika ajali ya Lucky Vicent kurejea nchini