Bingwa wa ngumi wa Taifa uzito wa Supper Middle, Twaha Kiduku amesema kuwa anataka kupanda ulingoni na mbabe mwenzake, Hassan Mwakinyo ili kumpata mbabe halisi wa Tanzania.

Akizungumza katika mahojiano maalum na Dar24 Media baada ya kumpiga Dullah Mbabe, Kiduku amesema kuwa ameamua kupanda ulingoni na Mwakinyo kutokana na matakwa ya mashabiki wa ndondi.

“Kuhusu Mwakinyo, mimi sikutaka kumuwaza au kumfikiria lakini wadau na mashabiki wangu wanahitaji wamtambue bingwa wa Tanzania ni nani. Kwahiyo, na mimi napenda sana kuwasikiliza mashabiki wangu kile wanachotaka, wakaniambia jana baada ya kumpiga Dullah Mbabe… ‘bro bwana tunamtaka Hassan’, na mimi nikamwambia bwana ulipo njoo tumalize hapa,” Kiduku ameiambia Dar24 Media.

Mwakinyo yuko kwenye kilele cha mafanikio ya masumbwi Tanzania, akiwa na rekodi nzuri tangu alipoishangaza dunia kwa kumpiga Sam Eggington katika ukumbi wa Birmingham nchini Uingereza, mwaka mmoja uliopita. Wiki chache zilizopita alimchakaza mkongo Kayembe Tshibangu.

Kiduku alieleza kuwa anaweza kupunguza uzito wake hadi kilo 69 ili awe na sifa za kupigana na Mwakinyo kwani amewahi kufanya hivyo awali.

Angalia mahojiano haya kwa kina hapa:

Gari linalopaa lafanikisha safari ya kwanza Japan
Habari kubwa kwenye magazeti leo, Agosti 30, 2020