Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amesema hati 214 zimetayarishwa kwa ajili ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam waliosalimisha ofa zao za umiliki wa ardhi kwenye wizara hiyo ili waweze kumiliki  ardhi hizo kihalali.

Waziri Lukuvi amesema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari juu ya mambo mbalimbali yanayohusu wizara hiyo Februari 27, 2017.

Waziri Lukuvi amesema kuwa ni rahisi kwa wananchi wenye umiliki wa ofa kutapeliwa kuliko wakiwa na umiliki wenye hati ambazo ni halali hivyo ili kuondoa changamoto hiyo wizara ilitoa muda kwa wananchi kupeleka ofa hizo ili watayarishiwe hati halali.

“Kuwa na umiliki halali wa ardhi ni jambo kubwa kwa usalama wa wananchi wenyewe, nataka ifike siku Tanzania iwe haina mtu anayemiliki ardhi kwa kutumia ofa kwa sababu sasa hivi wizara haitoi ofa, ofa hizo zilishakoma siku nyingi,”alisema Lukuvi.

Amesema ingawa muda wa kusalimisha ofa hizo za umiliki umekwisha lakini wizara hiyo inatoa muda zaidi kwa watu ambao bado hawajapeleka ofa zao katika Halmashauri zao za wilaya kupeleka ofa hizo ili waweze kumiliki ardhi hizo kwa hati.

Pia, Waziri Lukuvi amesema kuwa tayari Kampuni ya Kifaransa iliyoshinda tenda inaendelea na kazi na mnamo Julai mosi mwaka huu hati ya kwanza ya kielektroniki ya mfano itatolewa.

Amesema jengo litakalotumika kwa ajili ya shughuli hizo tayari limeshakamilika na mfumo huo bado unaendelea kutengenezwa ili kuwezesha wananchi wote wanaomiliki ardhi Tanzania wanamilikishwa hati za kielektroniki.

MKwasa: Hali Ya Kifedha Sio Nzuri Young Africans
Chadema yaweka ulinzi mkali nyumba ya mama Wema