Lebo ya kimataifa ya muziki ya Wanene Entertainment, imedhamini uwepo wa tuzo ya Video Bora ya Muziki Afrika Mashariki, katika Tamasha la Filamu la Kimataifa la Zanzibar (ZIFF) litakaloanza kufanyika Julai 8 mwaka huu visiwani humo.

Akizungumza na waandishi wa habari katika tukio la kusaini mkataba kati ya pande hizo mbili, Mkurugenzi wa Wanene Entertainment, Darsh Pandit alisema kuwa udhamini wa tuzo hiyo kwao ni ishara ya hatua kubwa kwani wameweza kufanikisha kitu kikubwa ndani ya muda mfupi tangu walipoanza kufanya kazi za muziki nchini.

Alisema Wanene watahusika katika kuandaa video mpya ya mshindi wa tuzo hiyo, video ambayo itakuwa na ubora na uhalisia wa eneo la Afrika Mashariki.

Wanene Entertainment ni lebo kubwa zaidi ya muziki Afrika Mashariki ambayo inahusika na kufanya kazi za wasanii kwa ubora wa kimataifa ikiwa ni pamoja na mastering na kutayarisha video.
Mkurugenzi wa Masoko wa ZIFF, Isihaka Mlawa ameiambia Dar24 kwenye mahojiano maalum kuwa hatua ya Wanene Entertainment ni mfano wa kuigwa kwani imesaidia kuinua video za muziki wa wasanii wa Afrika Mashariki wanaotangaza asili ya eneo hilo.

Alisema kuwa vigezo vya tuzo hiyo viliwekwa kwa ushirikiano wa ZIFF na kituo cha runinga cha kimataifa cha Trace ambacho ni wadhamini wakuu wa tuzo hiyo na kuzipata video tisa za wasanii wa Tanzania, Kenya na Uganda.

“Trace Music walikuwa na vigezo vyao ambavyo waliviangalia katika kuchagua hizi video na sisi tulikuwa na vigezo vyetu. Miongoni mwa vigezo hivyo ilikuwa ni pamoja na Location (eneo ambalo video imefanyika) pamoja na production (utayarishaji),” Mlawa ameiambia Dar24.

“Kwahiyo tulikuwa tunaangalia kwamba location ya hizi video lazima iwe ndani ya mipaka ya Afrika Mashariki, na watayarishaji wawe wametoka Afrika Mashariki hasa Tanzania. Lengo letu ni kuwaweka kwenye matamasha ya kimataifa watayarishaji wa muziki wa hapa nyumbani, na pia kuchagiza kuitangaza sekta ya utalii,” aliongeza.

Alisema kuwa ZIFF wangependa kuona video za wasanii wa Tanzania zikifanyika pia kwenye maeneo ya utalii ili ziweze kuchagiza kuwavutia wageni wanaoangalia video hizo kupitia vituo mbalimbali vya runinga, kuitembelea Afrika Mashariki.

Video tisa zilizochaguliwa kushindania ‘Trace Best East African Video Music Award’ ni:
Kutoka Tanzania:
Natafuta Kiki – RayVan
Uminikamata – Jux
Muziki – Darassa ft. Ben Paul
Kutoka Kenya
Uko – Avril
Now you know – Nyanshiski
Evarlast – GudiGudi
Problem – NaiBoi
Kutoka Uganda
Jubilation – Eddy Kenzo
Sheebah Karungi – Nkwatako
A Pass – Gamululu ft. Konshens

Kambi iliyokuwa ikihifadhi na kutumikisha watoto yateketezwa kwa moto Manyara
50 Cent aichafua albam mpya ya Jay Z, adai hawezi kushindana...