Kuna mambo unatakiwa kuyaomba kwenye maisha yako, kuna filamu ukisimuliwa utatamani kukutana na mastaa waliocheza filamu hizo upige nao picha. Hasa filamu hizo zikiwa zimechezwa na warembo, kama ile Angelina Jolie kwenye Mr.& Mrs. Smith; au Priyanka Chopra kwenye Don 2.

 Lakini wapo wanawake ambao unapaswa kuomba tu usikutane nao. Hata kama ni warembo na wana sura za kuvutia, basi ibaki tu kuwa unasikia wanayoyafanya ambayo hata waliojaribu kuyaigiza kwenye filamu walishindwa kuyaweka kama yalivyo…. Maana hayafanani na ubinadamu. Hawa ni wa katika karne ya 20 na 21.

Leo tunakupa orodha ya wanawake sita wahalifu na waliokuwa wahalifu hatari zaidi, ambao unapaswa kuwaweka kwenye maombi yako usikutane nao au usikutane na wanaofanana na hao na ukawa ndiye mlengwa wao.

Unaweza kuangalia/ kusikiliza hapa, au kuendelea kusoma hapo chini:

6. Phoolan Devi aka Bandit Queen

Ni Mhalifu hatari zaidi na mwanamke aliyekuwa anaogopwa zaidi nchini India. Alifanya matukio mengi makubwa ya kihalifu, aliua na aliteka watu wengi.

Alitikisa ardhi ya India, kuanzia miaka ya 1970 hadi 1990, alipoacha uhalifu, na akatua bungeni kama mwakilishi wa wananchi.

Phoolan Devi alikuwa mwanamke nunda na katili kwelikweli. Moja kati ya matukio yaliyowahi kutikisa, ni pale alipovamia kijiji cha Behmai, Rajput kwa lengo la kulipiza kisasi. Devi aliwahi kubakwa na kundi la wanaume kwenye hicho kijiji, akanusurika kuuawa, akakimbia.

Februari 14, 1981 majira ya jioni alirejea kulipa kisasi. Aliporejea aliteka kijiji kwa muda, akawataka wanakijiji wawatoe waliomtesa. Kisha akiwa na kundi lake, wakawakamata wanaume 22 alioamini walihusika katika tukio la kumbaka, akawapanga mstari na kuwaua wote kwa risasi kisha akatokomea.

Baada ya miaka kadhaa ya matukio na kutafutwa na polisi, aliamua kujisalimisha polisi; na kufunguliwa mashtaka kibao yakiwemo ya mauaji. Alikaa rumande kwa miaka 11, lakini baadaye alifutiwa mashtaka yote. Huwezi amini, mhalifu huyu wa zamani alichaguliwa kuwa Mbunge mara mbili na akawatumikia wananchi! Nadhani wengi walivutiwa tu na jinsi alivyowaua waliombaka.

Julai 25, 2001, Phoolan Devi aliuawa kwa kupigwa risasi na watu watatu waliokuwa wamejifunika sura zao. Alipigwa risasi tisa, kichwani, mkononi na kifuani. Mlinzi wake pia alipigwa risasi kadhaa.

Kupata picha kidogo tu, kaangalie filamu ya Bandit Queen ambayo staring wake ni Seema Biswas, wao wameigiza maisha ya Phoolan Devi.

5. Santokben Sarmanbhai Jadeja

Alipewa jina la ‘God Mother’. Huyu ni mwanamke ambaye alitesa kuanzia mwaka 1987 hadi 1996, raia wa India aliyezaliwa na roho nzuri na akaanzisha familia. Lakini, baadad ya mumewe kuuawa, roho ikachafuka, akabadilika na kuwekeza katika kuwasaka wauaji kwa lengo la kulipa kisasi.

Alianzisha kundi kubwa la kihalifu, na kila mpiganaji wake alimlipa na kumpa zawadi anapofanikiwa kumuua mtu mmoja kutoka kwenye kundi hasimu. Hatua hiyo ilisababisha kundi lake kufunguliwa kesi zaidi ya 500 wakiwa mafichoni, wakipiga kazi ya kulipa visasi. Katika kesi hizo, kulikuwa na kesi 14 zinazohusu matukio ya mauaji.

Lakini baada ya kupitia hatua za kisheria, aliyamaliza. Mwaka 1990 wananchi walimchagua kuwa mbunge kwa kipindi cha miaka mitano.

Ukiangalia filamu iitwayo ‘Godmother’, inaongelea maisha yake. Ingawa yeye mwenyewe alieleza kutopendezwa na filamu hiyo.

4.  Nisreen Mansour Al Forgani

Huyu alikuwa mmoja kati ya wanawake makomando wa aliyekuwa Rais wa Libya, Muammar Gaddafi. Cha kushangaza alikuwa msichana mdogo tu. Mwaka 2011 alikuwa na umri wa miaka 19 tu. Alikuwa hawezekani kuanzia kupiga ngumi (martial arts), na balaa lake zaidi ni anaposhika silaha. Alikuwa mdunguaji hatari sana na aliwateka waasi wengi peke yake. Alikuwa msichana mrembo aliyelazimishwa kuwa mpiganaji, akafanya zaidi.

Anakumbukwa kwa madai kuwa alikuwa nyenzo ya mauaji ya jeshi la Libya. Aliwahi kuwaua wafungwa 11 waliokuwa waasi, aliwapiga risasi mmoja mmoja akiwa kwenye chumba maalum. Kabla ya kujiunga na jeshi kwa shinikizo, Nisreen ambaye alizungumza akiwa hospitalini baada ya kifo cha Gaddafi, alisema alikuwa mcheza muziki tu (dancer).

Nisreen Mansour Al Forgani (katikati)

Lakini alipopata mafunzo makali jijini Tripol, alikuwa sniper hatari, alitumia silaha nyingi na alikuwa anajua kupiga ngumi. Akawekwa kuwa mlinzi nje ya Ikulu ya Libya kwa muda. Anasema wakati wa mafunzo alifundishwa kuwa hata mama yake mzazi akiigeuka Serikali ya Gaddafi anapaswa kumuua mara moja.

“Nilifundishwa, usipomuua adui atakuua wewe.”

3. Samantha Lewthwaite aka The White Widow

Huyu anaitwa ‘The White Widow’, yaani Mjane Mweupe. Ni mwanamke gaidi, mwanafamilia wa kundi la Al Shabaab la Somalia, mmoja kati ya watu wanaotafutwa zaidi duniani.

Alianza kutajwa kuanzia mwaka 2005, ambapo ilibainika kuwa alikuwa mjamzito, lakini alitekeleza mauaji akishirikiana na mumewe Germaine Lindsay. Wawili hao walishirikiana kuandaa na kutekeleza mashambulizi ya mabomu Julai 7, 2005 jijini London. Baada ya mumewe kufa, yeye alishiriki kufanikisha mashambulizi mengi ya kigaidi, akilipua mabomu kadhaa nchini Kenya.

Daily Mail iliripoti kuwa mwanamke huyu aliandika akisema kuwa anatamani hata mwanaye atakayezaliwa afuate nyayo zake za kigaidi.

2. Kate Barker

Turudi karne ya 20, katika miaka ya 1935, alikuwepo mama mmoja anayeitwa Kate Barker, wengine walimfahamu kama Arizona Barker au Arrie Barker. Wahalifu huwa wana majina mengi bana.

Huyu alikuwa chuma na nusu. Kwa mujibu wa FBI, alikuwa ‘mastermind’ wa kundi la kihalifu la familia. Yaani alikuwa anawaongoza vijana wake wa kuzaa kufanya uhalifu mkubwa. FBI walimtaja kama adui wa taifa au adui wa umma (public enemy). Matukio yao ya kihalifu, uporaji na mauaji yalifanya FBI kuumiza sana kichwa wakiwasaka. Kila alipoenda alienda na vijana wake wa kiume.

Mkurugenzi wa FBI, John Edgar Hoover alimtaja kama mama hatari zaidi na mpika matukio ya kihalifu hatari zaidi katika muongo wa mwisho wa mwaka 1930.

SHELLEY WINTERS Film ‘BLOODY MAMA’ (1970) Directed By ROGER CORMAN 24 March 1970 CTB7888 Allstar/Cinetext/AIP **WARNING** This photograph can only be reproduced by publications in conjunction with the promotion of the above film. For Editorial Use Only

FBI walifanikiwa kuwakuta kwenye nyumba moja familia hii ya kihalifu. Inaelezwa kuwa kulitokea tukio la kushambuliana kwa risasi kati ya mama na watoto wake dhidi ya FBI, majibizano ya risasi yalichukua muda mrefu sana kabla ya watuhumiwa wote kuuawa.

Naye amekuwa akitajwa kwenye filamu nyingi na nyimbo nyingi zinazooenesha mama mhalifu.

  1. Bonnie Elizabeth Parker

Bonnie Parker, alikuwa mmoja kati ya wanafamilia wawili wa ile ‘Bonnie and Clyde’, walikuwa wapenzi maaarufu waliotekeleza matukio mengi ya mauaji na uporaji, katika miaka ya 1930 nchini Marekani. Kati ya matukio aliyoshiriki, ni pamoja na kuiba magari, kuvamia vituo vya mafuta na kuiba fedha, kuvamia benki na migahawa na kufanikiwa kuiba. Matukio hayo waliyafanya Texas, Oklahoma, New Mexico na Missouri.

Mbaya zaidi, waliwahi kuvamia vituo vya FBI na Polisi, wakawatoa wafungwa watano kutoka Gereza la Eastham State la Texas. Walimteka mkuu wa kituo cha polisi na wakafanya walichotaka kufanya kituoni hapo na wakaondoka salama.

Baada ya kusakwa kwa udi na uvumba kwa miaka miwili, polisi waliwaua wote baada ya kuvamia maficho yao kwa kushtukiza huko Louisiana. Aliyewapa polisi taarifa ni rafiki yao wa karibu.

Maisha ya wawili hawa yamewekwa kwenye filamu ya Bonnie and Clyde ya mwaka 1967 na series ya Bonnie and Clyde yam waka 2013. Jay Z na Beyonce nao walitumia majina yao kutengeneza wimbo maarufu wa mapenzi wa ‘Bonnie and Clyde. Unaambiwa hakuna aliyekuwa anaomba kukutana na Elizabeth Parker.

Wapo wanawake wengi kwenye orodha, lakini hawa walikuwa hatari aisee katika karne ya 20 na 21.

Dkt.Gwajima kumuwakilisha Rais Samia Kongamano la Tatu la Kimataifa la Wanawake-Urusi
Sekta zaidi nchini kunufaika na mikopo nafuu