Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amepokea michango ya sh. milioni 40 kutoka kampuni ya ujenzi ya CHICO ya China ambao wametoa kiasi cha sh. milioni 20 na sh. milioni 20 nyingine zimetoka kwa Umoja wa Wafanyabiashara na Wenye Viwanda wa India waliopo nchini (India Business Forum) kwaajili ya kuwasaidia waathirika wa tetemeko Kagera.

Akiwasilisha mchango wake, Mwakilishi Mkuu wa kampuni ya CHICO hapa nchini, Guo Zhijian alisema wamesikitishwa na maafa yaliyotokea mkoani Kagera. “Tumefanya miradi mingi mkoani Kagera ikiwemo ujenzi wa barabara za urefu kilometa 300, kwa hiyo mkoa huu tunaujua zaidi. Tunatoa pole kwa wote waliopatwa na maafa  hayo,” amesema.

Naye Mwenyekiti wa umoja wa wafanyabiashara na wenye viwanda kutoka India (IBF), Bw. Gagan Gupta alimweleza Waziri Mkuu kwamba wameshtushwa na tukio hilo na kwamba wametanguliza kiasi hicho ili kisaidie juhudi za Serikali katika kukabiliana na maafa hayo.

Waziri Mkuu amewashukuru kwa misaada hiyo na kuahidi kuwa Serikali itahakikisha michango hiyo inafikishwa Kagera kwa walengwa.

Aidha, Majaliwa amewaomba wale walioahidi kutoa michango wakamilishe ahadi zao na wale walio mbali na benki watumie namba za simu zilizotolewa mahsusi kwa ajili ya kuchangia maafa hayo.

Akaunti ya maafa imefunguliwa katika Benki ya CRDB yenye namba 015 222 561 7300 kwa jina la KAMATI MAAFA KAGERASwiftcode: CORUtztz na namba za simu za mkononi zinazotumika kupokea michango hiyo ni 0768-196-669 (M-Pesa) au 0682-950-009 (Airtel Money) au 0718-069-616 (Tigo Pesa).

 

Vibali vya safari ni kero kwa Wabunge.
Tundu Lissu akwama Mahakamani, Dhamana yake hatarini