Leo Juni 19, 2017 Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amezindua Kamusi Kuu ya Kiswahili na uzinduzi huo umefanyika katika ukumbi wa Bunge mjini Dodoma.

Katika uzinduzi huo, Waziri Majaliwa amesema Serikali inatambua umuhimu wa lugha ya Kiswahili kwa ustawi wa Taifa na katika kulinda umoja wa Kitaifa.

“Serikali inatambua umuhimu wa lugha ya Kiswahili kwa ustawi wa nchi yetu na katika kulinda umoja wa Kitaifa. Hakika lugha ya Kiswahili ndiyo inayotufanya tuwe Watanzania. Hivyo, tunaithamini sana na kwetu hii ni lulu na tunu ya Taifa,” amesema.

Majaliwa amesema uzinduzi wa Kamusi hiyo unaenda sambamba na azma ya Serikali ya kutumia Kiswahili kwenye shughuli zote za kitaifa kama vile mikutano, mijadala, semina na ufundishaji shuleni.

Pia, Majaliwa ametumia fursa hiyo kumpongeza Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuhimiza matumizi ya Kiswahili kwenye mikutano na matukio muhimu ya kitaifa, kama vile dhifa za kitaifa anazowaandalia wageni wake kutoka nje ya nchi.

“Hata alipokuwa kwenye Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika wa mwaka 2017, Mheshimiwa Rais alitumia Kiswahili kuhutubia mkutano huo. Amekuwa akifanya hivyo, hata kwenye mikutano ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Lengo lake ni kuitangaza lugha hii ya Kiswahili,” alisema.

Akizungumza katika hafla hiyo fupi, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe amesema Kiswahili ni lugha ya pili inayotumiwa na watu wengi zaidi barani Afrika lakini pia ni lugha ya 10 kati ya lugha 6,000 zinazozungumzwa na watu wengi duniani.

Naye Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), Dk. Seleman Sewangi amesema kazi ya kuandaa kamusi hiyo ilianza Agosti 12, 2011 na kukamilika mwaka 2015 ambapo toleo la kwanza lilichapishwa.

Wydad Casablanca Kuamua Hatma Ya Al Ahly
Video: Uamuzi ya Mahakama kuhusu James Rugemalira na Harbinde Seth