Z Anto ambaye hivi karibuni alitajwa na Diamond Platinumz kuwa yeye pamoja na Kassim Mganga ndio watu wa kwanza waliomsikiliza na kumuunganisha na meneja wake wa kwanza, amefunguka anachokumbuka kuhusu hatua hiyo.

Kupitia mahojiano maalum aliyofanya wiki hii na Dar24, Z Anto amesema kuwa anamkumbuka Diamond aliyezungumza naye kwa mara ya kwanza akijitambulisha kuwa ni muimbaji na anataka asaidiwe kuunganishwa na Papaa Misifa; na kwamba iliiona nyota yake iking’ara kwenye kiwanda cha muziki alipokuwa anamsikiliza.

Alisema baada ya kuwaimbia mara tatu, walimrekebisha na kumshauri namna bora ya kuimba kisha wakampeleka kwa Misifa ambaye alikuwa anaogopa kuwekeza fedha zake kwa wasanii akihofia vipaji vyao kutomlipa. Hata hivyo, Z Anto na Kassim Mganga walifanya kazi kubwa mithiri ya mameneja masoko wa kipaji cha ‘Diamond’.

“Papaa alituuliza kwani nyie mmemsikiaje? Tukasema huyu jamaa ana nafasi nzuri ya kurudisha pesa yako. Ingiza pesa itarudi. Akasema ‘basi twendeni tukaongee ndani’, akampa Diamond nauli akaondoka,” alisema.

Mkali huyo wa ‘Binti Kiziwi’ alisema kilichoendelea ndani wakati wa mahojiano, kilimfanya ajiweke rehani ili kudhihirisha uhakika wa alichokiona kwa Diamond kuwa ni pesa.

“Tulipofika ndani alituhoji sana kama dakika 45 nzima, nikamwambia ndugu yangu pale ingiza hela na ukiingiza hela yako itarudi kwa asilimia 100, isiporudi nidai,” alifunguka.

Hata hivyo, Z Anto anasema haikuchukua siku moja kumshawishi Papaa Misifa kwani mara kwa mara walipokutana alikuwa akiuliza maswali ya kutaka uhakika kabla hajachukua uamuzi wa kuwekeza kwa Diamond.

Z Anto amefunguka pia kilichotokea baada ya Papaa kuanza kufanya kazi na Diamond na jinsi alivyosikia wimbo wake wa kwanza akiwa jijini Nairobi.

Aidha, amefunguka pia jinsi ambavyo alikuwa amemsahau hadi alipooneshwa picha yake na heshima aliyompa walipokutana baada ya miaka miwili, Diamond akiwa tayari yuko kwenye kilele cha kiwanda cha muziki nchini.

Angalia hapa video ya mahojiano hayo upate yote:

 

Serikali yatoa ufafanuzi wa taarifa ya balozi wa Umoja wa Ulaya ‘kufukuzwa’
Watu wasiofanya mazoezi hatarini kupata tezi dume