Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imekabidhi vifaa vya kujikinga na UVIKO-19 vyenye thamani ya milioni 57 kwa Mikoa 12 ya Tanzania Bara na 5 ya Zanzibar vilivyotolewa na Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania kupitia shirika la Kimataifa la Nutrition International (NI) ikiwa ni kuwakinga watoa huduma ya afya hususani katika zoezi la Utoaji wa Matone ya Vitamini A nchini.

Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo kwa wawakilishi wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI na Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mganga Mkuu wa Serikali Dkt Aifillo Sichalwe amesema vifaa hivyo vitaenda kuwasaidia watoa huduma za afya walio mstari wa mbele katika kutoa huduma za afya nchini bila kuwasahau watoa huduma za afya ngazi ya jamii (CHW)

Dkt Sichalwe amesema kutokana na changamoto ya UVIKO-19 Serikali inaendelea kuwapatia vifaa vya kujikinga na maambukiz ya UVIKO-19 Jumla ya Katoni 6000 za Barakoa (Mask) na Vitakasa Mikono (Sanitizer) lita 6000, vimetolewa na vitasambazwa katika mikoa 17 kwa watoa huduma waliopo katika vituo vya afya ili kuwawezesha kuendelea kutoa huduma za afya kwa ufanisi ikiwemo Kampeni ya utoaji wa Matone ya Vitamini A inayofahimika kama Huduma ya Mwezi wa Afya na Lishe ya Mtoto.

“Vifaa hivi vimeanza kutolewa katika mikoa 12 ya Dodoma, Geita, Kagera, Morogoro, Katavi, Mwanza, Kilimanjaro, Shinyanga, Simiyu, Singida, Tabora na Tanga pamoja na Mikoa yote mitano ya Tanzania Visiwani na mikoa hii imeteuliwa kwa sababu ilikuwa na ufanisi duni katika utoaji wa huduma za mwezi wa afya, hivyo kupitia msaada huu utasaidia kuimarisha kiwango cha katika utoaji wa huduma za matone ya Vitamini A kwa watoto wengi zaidi” Alisema Dkt.Sichalwe.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania Dkt. Ray Masumo ameishukuru Serikali ya Cananda kupitia Shirika lake la Nutrition International (NI) kwa kuendelea kuiunga mkono serikali katika vita dhidi ya UVIKO-19 na changamoto nyingine za Kilishe.

Dkt. Masumo amesema vifaa hivi vitawasaidia watoa huduma ya afya waliopo mstari wa mbele katika kutoa huduma za afya ikiwemo Huduma ya mwezi wa Afya na Lishe ya Mtoto kwani malengo yaliyopo ni kuhakikisha ifikapo Mwaka 2025 watoto wote nchini wafikiwe na huduma ya matone ya Vitamini A kupitia vituo vya afya vilivyopo nchini.

Nae Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Kimataifa la Nutrition International (NI) Dkt Daniel Nyagawa amesema wamechukua uamuzi wa kutoa vifaa kwa Serikali ikiwa kuunga mkono juhudi mbalimbali zinazochukuliwa katika kupambana na UVIKO-19 na wataendelea kushirikiana na katika afua nyingine ikiwemo zile za Kilishe ambazo shirika hilo limekuwa likizitekeleza hapa nchini.

Akipokea vifaa hivyo kwa niaba ya Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mkurugenzi wa huduma za Afya Dkt.Mwanahamisi Hassan amesema vifaa hivyo vitawasaidia watoa huduma za afya waliopo mstari mbele katika vita ya UVIKO-19 hivyo anawakaribisha wadau wengine kujitokeza katika kuunga mkono jitihada zinazochukuliwa na serikali katika vita hiyo.

Vurugu zazuka Bungeni Kenya
Bei mpya za kuunganisha umeme kuanza kutumika leo