Vijana Sita 6 wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Njombe kwa kosa la kughushi vyeti katika zoezi la usaili wa nafasi za kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa JKT.

Akizungumza na waandishi wa habari Mwenyekiti wa Kamati ya ulinzi na usalama mkoa wa Njombe ambaye ni mkuu wa mkoa huo, Christopher Ole Sendeka amesema kuwa kutokana na vitendo hivyo vya udanganyifu ikiwemo kughushi uraia wajumbe wa kamati hiyo wametengua nafasi za uteuzi za vijana walioteuliwa kujiunga na jeshi hilo na kusitisha zoezi la usaili na kutangaza kupokea upya maombi ya kujiunga na nafasi hizo.

“Baada ya kupitia wilaya moja na nyingine tumebaini kuwepo kwa udanganyifu wa vyeti kuanzia vya kuzaliwa, vya elimu ya msingi na tumegundua hata wengine uraia wao una mashaka, tumesitisha zoezi baada ya kujiridhisha kuwa taarifa zilizowasilishwa mbele yetu baadhi yake zina udanganyifu mkubwa, sasa tumetangaza upya vijana hawa walete maombi upya kuanzia tarehe 29 mpaka tarehe 8 mwezi wa 7, vijana hawa watapaswa kuwasilisha maombi yao kwa wakuu wa wilaya kila mmoja kwenye wilaya anakotoka,”amesema Ole Sendeka

Ameongeza kuwa licha ya vijana hao pia watu wote wanaohisiwa kuhusika katika vitendo hivyo vya udanganyifu watakamatwa na kuhojiwa ambapo wakigundulika hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

“Baada ya kufanya uchunguzi wapo vijana ambao tumeridhika wamegushi vyeti vyao, tumewaelekeza wakuu wa vyombo vya usalama katika mkoa, kuanza kuwashikilia vijana wale, na wale wote walio tajwa hivi sasa wako katika mikono ya vyombo vyetu kwa mahojiano zaidi,”ameongeza Ole Sendeka

Aidha, Wajumbe wa kamati ya Uinzi na Usalama wa mkoa huo wamesema kuwa wamefikia uamuzi huo kwa kuzingatia misingi ya sheria na haki ili kutoa nafasi kwa watoto wa wanyonge wakiwemo watoto wa wakulima.

Wiki mbili zilizopita mikoa yote nchini imeanza zoezi la vijana kupokea maombi ya vijana wanaojiunga na Jeshi la Kujenga Taifa katika ngazi za wilaya na baadaye kufanyiwa usaili katika ngazi za mikoa ili kupata vijana wanaostahili kujiunga na jeshi hilo.

Waziri Kairuki ahimiza ushirikiano kati ya kiwanda na wananchi
Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Juni 30, 2019