• Na Lilian Aidan Mahena

Wakati baadhi ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam wakiendelea kulalamikia kero mbalimbali zinazoletwa na mvua ikiwemo mafuriko na foleni kali katika baadhi ya barabara jijini humo, baadhi ya vijana wameichukulia hali ya mvua kunyesha kama fursa mpya.

Hali hii imeonekana kwa vijana wakazi wa Mbezi Beach, eneo la Goigi jijini humo, ambao wameonekana wakikusanya mchanga katika mitaro iliyopo kando ya barabara na kisha kuiingiza ‘sokoni’ kwa ajili ya kujipatia kipato.

Wakizungumza na Dar24, vijana hao walisema kuwa mvua zinaponyesha ni faida kwao kwani wanapata fedha za kujikimu kimaisha hadi shilingi 30,000 kwa siku.

“Tukishatoa huu mchanga kwanza tunasaidia mitaro kuwa wazi na maji kupita kwa urahisi na kuepusha mafuriko, lakini tunajipatia kipato hadi shilingi 30,000 kwa roli moja,” alisema mmoja kati ya vijana hao.

“Mimi hujipatia hadi shilingi 6,000 kwa siku baada ya kula wana.  Unajua sasa hivi hali ni ngumu, lazima uwe mbunifu hata katika kazi kama hizi ambazo zinaonesha kabisa kwamba tusipotoa mchanga yatatokea mafuriko barabarani lakini tunapata kitu pia kwa kujitolea,” alisema kijana mwingine aliyejitambulisha kwa jina moja la Omary.

Hata hivyo, vijana hao wamelalamikia kukosekana kwa vifaa vinavyoweza kuwasaidia kufanya kazi hiyo kwa ufanisi ili kuisaidia manispaa na wakazi wa eneo hilo bila kupata madhara.

“Ingawa hii ni fursa kwetu na msaada wa wakazi wa eneo hili, tunapata changamoto kubwa ya kuugua fangasi, tunatamani kuwa na vifaa ili tulinde pia afya zetu,” alisema Maximo.

Mvua zinazoendelea jijini humo zimesababisha kero na changamoto ya miundombinu katika baadhi ya maeneo ikiwa ni pamoja na kuharibu makazi.

Lil Wayne afunguka kuhusu mpango wa kujiunga na lebo ya Jay Z
Uongozi Simba wateta na Waziri Mwakyembe