Serikali imeandaa mradi utakaowanufaisha vijana milioni nne kufikia mwaka 2021 kwa kutumia rasilimali mbalimbali ikiwa ni pamoja na ardhi.

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu; Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Anthony Mavunde ameliambia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa mradi huo umeanza kutekelezwa. Ameeleza kuwa takribani vijana 32,563 wameshafaidika na mradi huo katika kipindi cha Mwaka wa Fedha 2018/19.

“Kupitia mradi wa Kuwezesha Ujuzi kwa vijana, tumefanikiwa kuwafikia vijana 32,563 katika kipindi cha Mwaka wa Fedha 2018/19, kwa ujumla tutawafundisha vijana milioni nne kurasimisha miradi yao hadi kufikia mwaka 2021,” alisema Mavunde.

Naibu Waziri huyo alieleza kuwa Serikali kupitia halmashauri za wilaya imetenga ardhi kwa ajili ya vijana hususan vijijini kwa ajili ya miradi ya kilimo.

Ameongeza kuwa wameshafanya mazungumzo na makampuni mbalimbali ili waanze kununua malighafi kutoka kwa makundi ya vijana yaliyoanza kutekeleza miradi ya kilimo.

“Tumefanikiwa kufikia makubaliano na Kiwanda cha Sayona. Hivi sasa vijana hao wako huru kuuza matunda yao kwa Sayona kwa ajili ya kutengeneza juisi. Tunafanya mazungumzo pia na Bakhresa kuona kama wanaweza kuanza kununua matunda kutoka Muheza [Tanga],” aliongeza.

Naibu Waziri huyo alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Fatma Hassan Taufiq (CCM), aliyetaka kufahamu mpango wa Serikali katika kuwasaidia vijana vijijini ili kupunguza idadi ya vijana wanaohamia mijini.

LIVE: Yanayojiri Bungeni jijini Dodoma leo Juni 12, 2019, maswali na majibu
Trump adai yuko tayari kufanya mazungumzo na Kim Jong Un