Mwenyekiti wa Chama cha wataalamu wa magonjwa ya akili Issack Lema amesema vijana wanaongoza kupata magonjwa ya akili huku sababu kubwa ikiwa ni msongo wa mawazo na matumizi ya vilevi.

Amesema hayo wakati akizungumza na Dar24Media kuhusu maadhimisho ya Siku afya ya akili leo Octoba 10, 2021 ambapo amesema kuwa vijana wengi wanapokutana na changamoto hawatafuti wataalamu wa kuwasaidia badala yake hujiingiza katika matumizi ya madawa ya kulevya na unywaji mkubwa wa pombe.

”Kutafuta suluhu ni hatua muhimu sana ya kukabiliana na magonjwa ya akili lakini je, suluhu hiyo unaitafutaje? wengine wanaona matumizi ya vilevi ndiyo suluhu lakini kumbe wanajiangamiza na kupata matatizo mengine makubwa zaidi” amesema Lema

Aidha amesema kuwa ni vyema watu wanaokumbana na changamoto mbalimbali wakawaona wataalamu wa afya ili waweze kusaidiwa na kwamba miongoni mwa changamoto zilizopo ni miundombinu kwa maana ya hospitali za kutosha za kutibu maradhi hayo pamoja na uhaba wa wataalamu.

Lema amesema changamoto nyingine ni kutokuelewa kama wanaumwa na pia kujinyanyapaa wenyewe.

”Wengine wanaamini kuwa wamerogwa au laana kuna tatizo pia la jamii kwanyanyapaa hawa wagonjwa, wengine hawazingatii matibabu wengine, wengine uchumi wao ni mdogo kumudu gharama za matibabu”

Pambano zito: Tyson Fury alivyompiga Wilder kwa KO
Habari kubwa kwenye magazeti leo, Oktoba 10, 2021