Vijana nchini wametakiwa kuachana na biashara ambazo zimekuwa zikiwapotezea muda na badala yake wajikite katika ubunifu wa kazi wanazozifanya, ili kuweza kupata matokeo chanya yatakayobadilisha maisha yao.

Hayo yamebainishwa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Beng’i Issa, katika uzinduzi wa shughuli za kiubunifu Kitaifa zilizofanyika jijini Dodoma, zilizoandaliwa na Tanzania Innovation Explore Gala.

“Epukeni biashara zinazowapotezea muda, haiwezekani miaka mitano unafanya biashara isiyokupa faida, jitahidini katumia ubunifu wa kazi ambazo zitawafanya mfikie malengo yenu, maana kama utajibidiisha katika ubunifu ni lazima utayapata mafanikio,” ameongeza Beng’i.

Amesema wengi wa Vijana wamekuwa hawana mawazo mbadala katika kujikwamua na hali ngumu ya kiuchumi inayowakabili kwa kuendelea kung’ang’ania mfumo mmoja wa mbinu za kibiashara ambazo haziwaingizii faida na mwisho huitupia lawama Serikali au mashirika ya utoaji mikopo.

 Beng’i ambaye alikuwa mgeni rasmi katika ufunguzi huo amebainisha kuwa uzoefu unaonesha baadhi ya watu wanaoendesha biashara kwa mikopo wamekuwa hawafikii malengo yao kutokana na faida kidogo wanayoipata huku wakitakiwa kufanya marejesho.

“Mtu huna mbinu za biashara zilizo na mashiko halafu unachukua mkopo ni wazi kuwa utaanguka tu, hivyo ni lazima kuweka mawazo mbadala ambayo kibiashara yanaweza kukupa faida kwa kuwa mbunifu katika bidhaa zako,” ameongeza Beng’i.

Kwa upande wake Afisa maendeleo ya jamii Idara kuu ya Vijana Jiji la Dodoma Mfungo Daniel Manyama, amesema ili kupata maendeleo yenye muonekano chanya maishani, Vijana hawana budi kutumia Elimu walizonazo kwa kuleta ubunifu na kujiajiri.

Amesema utafutaji na uzalishaji wa mipango thabiti ikiwemo suala la ushirikishwaji wa mawazo ya Vijana kwa watu sahihi, utaleta utatuzi wa changamoto na kupata mafanikio kwa kila kijana mpambanaji, aliye na kiu ya maendeleo.

“Elimu hii tuipatayo mashuleni inatakiwa itusaidie katika suala la ubunifu na kujiajiri maana kuwa na elimu halafu haitumiki katika kupata mbinu mpya za ubunifu inakua haina mantiki, sasa sisi kama eneo la uwezeshaji watu mbalimbali hasa vijana katika vikundi vyao tupo tayari kuunga mkono juhudi zenu,” amesema Manyama.

Awali akiongea katika uzinduzi huo mwakilishi wa makundi ya Vijana toka chuo cha Mipango Dodoma (IRDP), Gabriel Muhuwa amesema uwezo wa kubuni na kuwa na vipaji mbalimbali utasaidia kuinua uchumi wa wajasiriamali wadogo ambao wamekuwa na kiu ya kupata mafanikio.

Suala la kukuza mitaji inayotokana na ufanyaji wa biashara kwa wajasiriamali mbalimbali limekuwa likilalamikiwa katika maeneo mengi nchini kutokana na baadhi yao kukosa ubunifu, kuwa na uelewa mdogo wa mambo ya kibiashara, kutoitumia ipasavyo elimu waliyoipata katika ubunifu na kukosa maarifa mapya.

Mbappe kuzikosa Iceland, Uturuki
Waarabu kuamua hatma ya Young Africans kimataifa