Vijana wa kitanzania na Afrika kwa ujumla wametakiwa kuitii na kuirithi misingi ya amani iliyoanzishwa na Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliekuwa muasisi wa Harakati za Muungano wa Afrika.

Hayo yamesemwa na Wakili Sabelo Sibanda kutoka Afrika Kusini ambae ni mgeni Rasi katika Kongamano la siku ya kumbukizi ya mwalimu Nyerere katika Chuo cha ufundi Veta Chato Geita.

Wakili Sibanda amesema Mwalimu Nyerere alianzisha harakati za Muungano wa Afrika na sera ya Ujamaa kama sera muhimu kwa Watanzania ambayo inatakiwa kuwafanya watanzania kuona kuwa hakuna raia wa kigeni atakaekuja Tanzania na Afrika kuleta maendeleo Zaidi ya  Watanzania wenyewe.

“Leo ambavyo tunamkumbuka Mmoja ya watu muhimu kwa Taifa la Tanzania naongea na watu waliokuwepo enzi za uongozi wake na Vijana ambao wanasikia habari zake tusahau hii dhana mbovu ya kuona kuwa kuna watu wa nje ya nchi kama china, Uingereza na kwingineko ambao wanaweza kuja na kusaidia kufanya mambo ya maendeleo, hata hizo fedha za misaada wanazotoa ni kwa sababu wanapata faida kadhaa wao” amesema Sibanda

Wakili Sibanda ameongeza kuwa Ni muhimu waafrika waanze kurudia sera ambazo Mwalimu Nyerere alizianzisha kwa sababu zote zilikua zinasaidia Tanzania na Afrika kujiinua kiuchumi, na kuwanyanyua watu, na kusaidia watu wa bara zima la Afrika.

Wakili Sibanda amewaasa Waafrika na hasa Vijana waangalie Maamuzi yao ya sasa katika maisha na uongozi kama yanaipeleka nchi mbele zaidi kwenye uhuru au yanarudisha nyuma kwa mabeberu.

Amesema Mwalimu Nyerere alikua anatupeleka mbele na kujitoa kwa mabeberu ila kwa sasa viongozi vijana wanatafuta mahusiano na misaada kwa watu wa nje bila kujali sera za uhuru zilizoanzishwa na Waasisi hali inayorudisha nyuma kwa mabeberu.

“Mwalimu Nyeyere Pamoja na Marehemu Magufuli walikua sio tu watanzania bali walikua ni Watoto wa Afrika na waliweka Sera ambazo zinaleta maendeleo kwa Afrika nzima bila kujali misaada ya kifedha ndio maana hawakuhangaika na yote yaliyokua yanasemwa na mataifa ya kigeni”.

Amewataka Vijana wajiulize binafsi kumkumbuka Mwalimu Nyerere kwa miaka hii 22 ina faida ipi kwa mtanzania na muafrika na kama kumkumbuka kunasaidia maendeleo ya Nchi na Bara hili na kuleta mabadiliko katika maeneo yanayohitaji msaada.

“Wakati wa kupigania uhuru vijana wa umri kama wenu walikua wamebeba silaha vitani na kupigania mipaka ya Tanzania na uhuru wa nchi yao Je nyie mnafahamu lengo la uwepo wenu kwa nchi yenu na maendeleo yake”? amesema Sibanda

Kongamano la siku ya kumbukizi ya mwalimu Nyerere limefanyika katika Chuo cha ufundi Veta Chato Geita lenye kauli mbiu “Amani yetu ndio utamaduni wetu na Umoja wetu ndio Urithi wetu ni kwanmna gani urithi huu tunaurirhisha kwa Vijana”?

Jamii yaaswa kukabiliana na magonjwa yasiyo ambukiza
RC Makalla aagiza ofisi za Serikali za Mitaa na Kata kuwa na Mgambo