Vijana wameaswa kuwekeza elimu zao katika sekta ya kilimo ili kuweza kutatua changamoto ya ajira ambayo imekuwa ni kilio kwa vijana wengi wakitanzania.

Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Kilimo, Innocent Bashungwa katika uzinduzi wa vitabu vilivyoandaliwa na taasisi ya Repoa inayojihusisha na mambo ya utafiti ambavyo vimelenga zaidi kuhusu kilimo, ambapo amesema kuwa vijana wanatakiwa wabadilike na wasome alama za nyakati hasa kutokana na mazao yaliyopo hapa nchini yanahitajika katika nchi za jirani ikiwemo Msumbiji, Malawi na mpaka nchi za Ulaya.

“Wakulima wetu wamekuwa wakizalisha mazao bila kujua wanauza wapi lakini ndani ya Serikali hadi sasa mtaona chini ya wizara ya kilimo kuna idara ya masoko kwaajili ya timu ya kutafuta masoko,” amesema Bashungwa.

Aidha, ameongeza kuwa anaweza akawa kijana si lazima akashike jembe anaweza akaanzisha kampuni ambayo imejikita katika masoko ya mazao ya wakulima wa hapa nchini na ikawa ajira kwako.

Katika vitabu ambavyo vimezinduliwa na Naibu Waziri vimelenga kutoa elimu juu ya kilimo pamoja na umwagiliaji hasa kutokana na tafiti ambazo walizifanya Repoa.

Hata hivyo, moja ya vitabu hivyo kimeelezea elimu na uzalishaji kwenye kilimo Vijijini, ambapo kimeandaliwa na Profesa Lucas Katera, kingine kimeeleza Tathmini ya mfumo wa kitaasisi wa maboresho wa Utumishi kwa Umma, ambacho kimeandaliwa na Dkt. Jamal Msami, wakati kingine kinazungumzia Mabadiliko ya kitaasisi na vikwazo vya Ushindani kwenye Masoko, ambacho kimeandaliwa na Dkt. Donald Mmari, cha mwisho ni kitabu ambacho kimezungumzia Sera za kilimo na jitihada za Kupunguza Umasikini Tanzania ambacho kimeandaliwa na Profesa Paschal B. Mihayo.

LIVE: Yanayojiri Bungeni Dodoma leo Mei 14, 2019
Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Mei 14, 2019