Ombi la Profesa Ibrahim Lipumba kurudia wadhifa wake kama Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF), huenda likagonga mwamba baada ya baadhi ya viongozi wa ngazi za juu wa chama hicho kupinga uamuzi huo.

Jana, Profesa Lipumba aliwaeleza waandishi wa habari kuwa amemuandikia barua Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad kuomba kutengua uamuzi wake wa kujiuzulu nafasi ya uenyekiti wa chama hicho alioufanya Agosti mwaka jana.

Akizungumzia uamuzi huo wa Profesa Lipumba, Naibu Katibu Mkuu Nassor Ahmed Mazrui amesema kuwa haoni sababu ya kumpokea kwani kilichomuondoa katika nafasi yake bado kipo.

“Sababu zilizomuondoa zingalipo. Kinachomrudisha ni nini? Alihoji Mazrui. “Anakuja kukiharibu chama,” anakaririwa katika sentensi nyingine.

Alienda mbali na kueleza kuwa mwanasiasa huyo mkongwe anatumiwa na CCM kuingia kukivuruga chama hicho wakati huu ambao wanaendelea kupambana kudai haki waliyoporwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana visiwani Zanzibar.

Nassor Ahmed Mazrui

Nassor Ahmed Mazrui

“CCM wanaona kinachoendelea, hivyo wameona wamtumie Lipumba kuja kuharibu mipango yetu. Hatuna muda wa kumjadili. Tunataka haki iliyoporwa,” alisema.

Naye Kaimu Mwenyekiti wa chama hicho, Twaha Taslima ameeleza kuwa haoni uwezekano wa Profesa Lipumba kurudi kwenye nafasi hiyo na kwamba ibara ya katiba ya chama hicho aliyoitumia ina tafsiri zaidi ya moja.

Mkurugenzi wa Mawasiliano wa CUF, Abdul Kambaya alitofautiana na misimamo ya viongozi hao na kueleza kuwa Profesa Lipumba anaweza kurudi katika nafasi yake iliyo wazi kwa mujibu wa Katiba ya chama hicho.

Mwanasiasa huyo aling’atuka nafasi yake baada ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kumkaribisha Edward Lowassa, mgombea urais kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema). Ingawa Profesa Lipumba ndiye aliyemtambulisha Lowassa mbele ya waandishi wa habari, alijiondoa baadae na kueleza kuwa amechukua uamuzi wa kujiuzulu kwa sababu moyo wake unamsuta.

Video: Mbunge anataka kupigiwa Saluti, Waziri Olenasha atoa agizo
Video: 'Lipumba aomba cheo chake CUF, Zitto atoa mazito kwa JPM' - Magazeti