Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima ametoa wito kwa Viongozi hususani wanawake kubeba ajenda ya kukabiliana na ukatili wa kijinsia na watoto kwenye vikao vyote kuanzia kwenye maeneo yao.

Waziri Dkt. Gwajima ametoa wito huo alipokuwa akiwasilisha mada ya mapambano ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto kwenye mafunzo ya Wajumbe wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) na Viongozi wa UWT ngazi ya Mikoa na Wilaya jijini Dodoma.

Amesema, Wanawake Viongozi wana nafasi ya kuzungumzia ajenda ya kutokomeza ukatili wa kijinsia na kwa watoto kwani, pamoja na takwimu kuonesha wanawake wanafanyiwa ukatili, kuna baadhi ya wanawake wanakatili watoto au wanakatili wengine au wanajikatili wenyewe.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima.

Aidha, Dkt. Gwajima amefafanua kuwa wapo baadhi ya wazazi au walezi wanawasuka watoto nywele tena kwa maumivu makali urembo ambao hauna tija kwa watoto zaidi unawasababishia athari kwenye ubongo jambo ambalo ni ukatili wa Wanawake kwa watoto wa kike huku akiwataka kuweka mikakati ya kupambana kutokomeza ukatili na malezi duni yanayochangia kuongezeka kwa vitendo vya ukatili.

Dkt. Gwajima, pia amesema utandawazi umekuwa changamoto inayoathiri mifumo ya malezi kuanzia nyumbani, shuleni na maeneo mengine hali iliyoathiri uimara wa mifumo ya wakala wa malezi ikiwemo familia, shule, Dini na jamii kwa ujumla.

Hata hivyo, Waziri Dkt. Gwajima ameipongeza mikoa ya Arusha, Mbeya, Kinondoni, Tanga na Mwanza kwa kuwa na mifumo imara inayotoa elimu kwa jamii na kufuatilia vitendo vya ukatili kwani katika kuelimisha jamii namna ya kuzuia na kutoa taarifa, ili hatua za kisheria zichukuliwe, kwani matukio mengi ya ukatili hufichwa na jamii maeneo ambako hakuna elimu na mifumo thabiti hivyo, manusura hukosa huduma na haki.

Halmashauri za Geita, GGML wasaini makubaliano Bilioni 19 CSR
Uchafuzi wa Mazingira: Serikali kukabili tabia za Binadamu