Viongozi tisa wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) pamoja na mwenyekiti wao taifa, Freeman Mbowe wanakabiliwa na kesi Mahakamani.

Hii inatokana na viongozi hao kutakiwa kufika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mara kwa mara kukabiliana na kesi yao inayowakabili ya uchochezi kwa kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja na nusu sasa.

Aidha, sehemu kubwa ya maisha yao yapo mahakamani kuliko majimboni au maofisini kwao wanakofanyia kazi na biashara zao mbalimbali.

Mbowe na vigogo wengine wanane wa Chadema walifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Machi 27, 2018 wakikabiliwa na mashtaka manane.

Mbali na Mbowe, viongozi wengine walioshtakiwa ni pamoja na Katibu Mkuu wa Chama hicho, Dkt. Vincent Mashinji, Naibu Katibu Mkuu bara, John Mnyika na Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu.

Wengine ni Ester Matiko mbunge wa Tarime Mjini, Halima Mdee mbunge wa jimbo la Kawe, Ester Bulaya mbunge wa Bunda Mjini, John Heche mbunge wa Tarime Vijijini na Peter Msigwa mbunge wa Iringa Mjini.

Kabla ya kufikishwa mahakamani vigogo hao walikuwa wakihojiwa polisi mara kadhaa toka Februari 2018 ulipofanyika uchaguzi mdogo Jimbo la Kinondoni baada ya kudaiwa kufanya maandamano yasiyokuwa na kibali, ambayo yalitawanywa na polisi.

 

 

Mkutano wa SADC wahitimishwa, JPM ataja waliyokubaliana
Video: Kasi ya maendeleo ya JPM yahamia SADC, Ajali ya Moro ilivyorejesha machungu ya mwaka 2000