Viongozi wa madhehebu ya dini hapa nchini wamemtaka Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda kumuomba radhi Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es salaam, Simon Sirro na kufuta kauli yake  kwa jeshi la polisi kuwa linapokea rushwa kutoka kwa wauza shisha.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Maadili, Amani na haki za binadamu kwa jamii ya madhehebu yote nchini, Askofu William Mwamalanga alipokuwa katika kongamano la viongozi wa dini.

Amesema kuwa kauli aliyoitoa Makonda imekosa  Maadili na hekima mbele ya jamii, kuwa inachochea na kuidhalilisha Serikali na inaweza kuwa chanzo cha chuki kati ya watendaji Serikalini

“Tunamkemea Makonda  kwa kauli yake, kitendo cha kumdhalilisha Kamanda Sirro na wenzake mbele ya hadhara ni utovu wa nidhamu na kielelezo cha ukosefu wa maadili” alisema Mwamalanga.

Aidha, ameongeza kuwa kitendo alichokifanya ni cha kumdhalilisha Rais Magufuli na kuongeza kuwa ni lazima kamanda Sirro aombwe radhi  kwani ni mtu mwadilifu na ni mfano wa kuigwa kwa makamanda wa polisi.

Hata hivyo Mwamalanga amewahimiza viongozi wa dini nchini kuwaombea askali polisi kutokana na kazi kubwa ya kupambana na panya road, wavuta bangi, wavuta shisha, wavuta unga, wahamiaji haramu na majangili wa pembe za ndovu.

NACTE kuvifungia vyuo vikuu 26
Gareth Southgate Awakuna Viongozi Wa FA