Wakati hatari ya kuzidi kusambaa kwa virusi vya Corona ikiongezeka nchini China, wafanyabiashara zaidi ya 200 wa Uganda wamefika katika ubalozi wa China jijini Kampala wakibembeleza kupewa VISA ili waende nchini humo kuendeleza biashara zao.

Hayo yamebainishwa na Waziri anayeshughulikia masuala ya Afya nchini humo, Robinah Nabbanja alipozungumza na vyombo vya habari hivi karibuni.

Waziri Nabbanja ameeleza kuwa alifanya mazungumzo na Balozi wa China nchini humo, na alimueleza wazi kuwa hali ni mbaya nchini kwao na imefikia hatua watu wanajitenga, huduma za umma zimesitishwa ikiwa ni pamoja na usafiri wa umma na huduma za migahawa kutokana na hofu ya kusambaa kwa Virusi vya Corona.

Alisema kuwa Balozi huyo aliwaeleza kwa masikitiko jinsi ambavyo wafanyabiashara hao walivyofanya kila jitihada za kupata VISA ingawa walielezwa wazi hali halisi.

“Kuna jamii ya Wafanyabiashara wa Uganda, hata hapa Kampala ambao wamekuwa wakifanya biashara zao kwa kufuata mizigo nchini China. Jana tulikuwa na mkutano na Balozi wa China na tulikubaliana kuchukua hatua kadhaa ikiwa ni pamoja na kuwachunguza wote wanaoingia nchini kupitia Uwanja wa Ndege,” alisema Waziri Nabbanja.

“Hata hivyo jana nilijikuta nashangaa sana, kwa sababu Balozi alisema ofisi yake ilikuwa imejaa watu zaidi ya 200 waliokuwa wanatafuta VISA ya kwenda China kufanya biashara! Nyie mko kwenye Whatsapp mmekuwa mkiona jinsi ambavyo watu wanaanguka ghafla.

“Lakini mfanyabiashara kwakuwa tu aliuza bidhaa zake zote Desemba anataka aende tena akanunue bidhaa nyingine China. Huko China usafiri wa umma umesitishwa, hivyo ndivyo Balozi alivyotuambia! Watu wanaishi kwa kujificha makwao. Hata migahawa imefungwa, wanaepuka mikusanyiko ya umma. Sasa wafanyabiashara wanataka kwenda huko China kwa kutoa muhanga maisha yetu sote [wakirejea]. Jamani kama China ambayo ni Taifa la pili lenye nguvu kiuchumi duniani limeshindwa kudhibiti hili janga, hivi likija hapa Uganda kweli tutaweza?” alihoji kwa mshangao.

Aidha, Waziri huyo alisema kuwa bado nchi hiyo iko salama na hakuna virusi vya Corona. Aliwataka wananchi wa Uganda walioko China kubaki huko waliko hadi mambo yatakapokuwa sawa, na walioko Uganda aliwasihi wasiende nchini China wakati huu.

Zaidi ya watu 1,000 wamepoteza maisha hadi sasa kutokana na maambukizi ya virusi vya Corona nchini China.

Jana pekee, watu 103 walipoteza maisha katika Jimbo la Hubei, takwimu za Serikali ya China zinaonesha kuwa hadi sasa watu 1,016 wamepoteza maisha. Maambukizi yamepanda kutoka 2,478 hadi 3,066.

Rais Magufuli amfuta kazi mtumishi aliyechana Quran
Corona yaathiri utalii nchini