Imefahamika kuwa Mshambuliaji kutoka nchini Serbia na klabu ya Fiorentina, Dusan Vlahovic, amefikia makubaliano binafsi na klabu ya Juventus, kabla ya kukamilisha uhamisho na wababe hao wa Ligi Kuu Italia, Serie A.

Vlahovic amekua akihusishwa na mpango wa kuwania na Arsenal katika Dirisha Dogo la Usajili, lakini mambo yamebadilika kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa nchini Italia.

Mwandishi wa Habari wa Italia, Giacomo Scutiero amedai Washika Bunduki hao hawana nafasi ya kumpata Vlahovic, kwa sababu tayari alikubali kujiunga na Juventus Oktoba, mwaka jana.

Scutiero pia amesema mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 21, ndiye mchezaji pekee ambaye Juventus wamejiandaa kumsajili kwa fedha nyingi mwezi huu au majira ya joto, huku Vlahovic akiwa na nia ya kusajiliwa na klabu hiyo hata kama watashindwa kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Meneja wa klabu ya Fiorentina, Vincenzo Italiano, anaamini Vlahovic anaendelea kuwa na ari ya kuichezea klabu hiyo ingawa mshambuliaji huyo amebakiza chini ya miezi 18 tu kwenye mkataba wake.

Vlahovic alifunga bao lake la 17 la Serie A msimu huu katika ushindi wa bao 6-0 dhidi ya Genoa mwanzoni mwa juma hili (Jumatatu), jambo ambalo linamfanya awe sawa na Ciro Immobile wa SS Lazio kileleni mwa msimamo wa mbio za kuwania Kiatu cha Dhahabu.

Klabu za Manchester City, Manchester United, Tottenham Hotspur na Real Madrid nazo zinatajwa kuwania Vlahovic.

Luis Suarez kurudi England
Simba SC kujifua Morogoro