Waandishi wa Habari kisiwani Pemba wametakiwa kutumia nafasi zao kuandika habari zinazolenga kuhamasisha vyama vya siasa na wadau mbalimbali kuwa na mpango wa kutoa elimu ya uraia mara kwa mara na kuacha kusubiri kipindi cha uchaguzi.

Wito huo umetolewa na mwezeshaji wa mafunzo ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari kisiwani Pemba kufanya uchambuzi wa habari zinazohusu wanawake, demokrasia na uongozi, Sabahi Mussa Said, ambayo yameandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ), ZAFELA pamoja na PEGAO  kwa kushirikiana na Ubalozi wa Norway nchini.

Sabahi amesema kwa muda mrefu taasisi mbalimbali hasa vyama vya siasa havifanyi utaratibu wa kutoa elimu ya uraia kwa wananchi hasa wanawake, jambo ambalo hupelekea wengi wao kushindwa kupata elimu ya kushiriki kupata haki zao za msingi.

“Mara nyingi elimu ya uraia hutolewa pale tu tunapokaribia kipindi cha
uchaguzi jambo ambalo kwa kweli huwakosesha sana wanawake kuelewa haki zao za msingi hasa kushiriki kwenye uongozi, hivyo ni wakati kwenu waandishi kulisemea hili ili wadau wote wanaohusika na hili waweke utaratibu wa kutoa elimu hii mara kwa mara hasa kwa wanawake na si kusubiri kipindi cha uchaguzi ndipo elimu hizi zianze kutolewa,” amesema Sabahi.

Aidha, Sabahi amesema kwamba kutokana na dhana potofu iliyojengeka ndani ya jamii juu ya mwanamke anayeonekana kuwa jasiri, na kwamba ni wajibu kwa vyombo vya habari kujikita katika utoaji wa elimu inayolenga kubadili fikra hizo.

Amesema, “Waandishi wa habari tunalo jukumu la kuelimisha jamii, kubadili fikra za kuamini kwamba mwanamke mwenye ujasiri wa kusimama na kuzungumza mbele za watu hana heshima.”

Kwa upande wake mwanaume wakala wa mabadiliko wa kuhamasisha jamii kubadili fikra juu ya dhana ya wanawake na uongozi, Mohammed Hassan Ali amewataka waandishi wa habari kuandaa habari zenye kulenga kupima ubora wa wanawake viongozi ili kuwahamasisha wengine.

Mshiriki wa mafunzo hayo, Time Khamis Mwinyi kutoka Redio ya Jamii
Micheweni amesema kuwepo kwa ajenda maalum katika vyombo vya habari kuhusu elimu ya wanawake na uongozi itasaidia kuongeza hamasa zaidi kwa wanawake kujitokeza kushiriki katika nafasi hizo.

Mradi wa kuwawezesha wanawake kushiriki katika masuala ya Demokrasia na uongozi unatekelezwa katika maeneo mbali mbali Unguja na Pemba ukiwa na lengo la kuwanufainisha wanawake 600.

Jafo awataka Zimamoto, Skauti wakomeshe majanga ya moto shuleni
Katibu Mkuu EAC kuchaguliwa kesho Februari 27