Katika jitihada za kukuza pato la mkulima Chama kikuu cha ushirika Mkoani Singida (SIFACU), kimetakiwa kuwasimamia kikamilifu wakulima kuondoa masalia ya miti ya zao la Pamba mashambani ili kukabiliana na wadudu waharibifu.

Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa mkoa wa Singida Dr. Rehema Nchimbi hii leo Novemba 4, 2019 katika kikao chake kilichowakutanisha Viongozi wa chama hicho na baadhi ya wakulima wa zao la Pamba mkoa wa Singida.

Amesema kutoa Masalia hayo mapema na kuyachoma Moto itasaidia kuondoa Wadudu shambani wanaoathiri zao hilo na hivyo kupelekea mavuno bora yatakayo msaidia mkulima kupata pesa za kukimu maisha na kuongeza pato la Taifa.

“Lazima tujenge uchumi ulio bora kwa kusimamia misingi ya uhai wa kilimo, simamieni wakuliwa ili kupambana na wadudu waharibifu na hakikisheni wanaondoa masalia ya miti mashambani itasaidia kupata mavuno bora,” amebainisha Dkt. Nchimbi.

Dkt. Nchimbi ameongeza kuwa vyama hivyo vinatakiwa kutimiza wajibu wao na kuleta ufanisi katika sekta hiyo badala ya baadhi ya watu kuendelea kuilaumu Serikali kwa mambo ambayo yanaweza kuchukuliwa hatua mapema na kuzuia uharibifu mashambani.

Aidha katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Mkoa ametoa muda wa miezi miwili ya Novemba na Disemba kwa vyama vyote vya Ushirika ambavyo havijakaguliwa vifanyiwe ukaguzi ili kupata takwimu halisi ya uhalali wa wake.

“Kuna watu wamejificha nyuma ya pazia kwa kutokamilisha mambo muhimu ya vyama na huu ni mpango mbaya ndani ya kipind kifupi yaani miezi hii miwili iliyobaki ya novemba na disemba vyama vyote vya ushirika viwe vimefanyiwa ukaguzi,” amesema Mkuu huyo wa Mkoa.

Awali Makamu Mwenyekiti wa chama kikuu cha ushirika Mkoa wa Singida (SIFACU), Yahaya Ramadhan akizungumza katika kikao hicho amesema wamekuwa wakiwasaidia wakulima kuungana na kushiriki mambo mbalimbali ili kuondokana na sintofahamu ya majawabu ya matatizo yanayowakabili.

Amesema katika kuhakikisha mkulima anapata huduma kwa wakati tayari wameongeza idadi ya vyama kutoka 36 hadi kufikia 66 na kuwakaribisha wale wote wenye nia ya kujinga na SIFACU na kwamba wamekuwa wakishirikiana na Halmashauri za Mkoa huo kuhakikisha wanasukuma mbele gurudumu la Kilimo.

“Lengo kuu ni kuhakikisha mkulima anapata faida na elimu katika kuboresha shughuli za kilimo na ndiyo maana kwa ukaribu tumekuwa tukifanya kazi na Halmashauri zote tano za Mkoa huu hivyo nisisitize umoja na ninawakaribisha wale wote wenye nia ya kujiunga na chama,” ameongeza Ramadhan.

Mwanahabari aliyepambana na Ebola auawa, Nyumba yachomwa moto
Mchungaji akamatwa na pembe za ndovu

Comments

comments