Sakata la vyeti feki limerudi kwa sura mpya kwa watumishi wa umma ambao wamedaiwa kukwamisha kukamilika kwa zoezi hilo, hali inayopelekea kukwamisha mpango wa kuongeza mishahara.

Akizungumza jana baada ya kusikiliza maombi ya Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta), Katibu Mkuu wa Menejimenti ya Utumishi wa Umma na utawala Bora, Laurian Ndumbaro alisema kuwa watumishi ambao bado hawajawasilisha vyeti vyao kwa ajili ya kuhakikiwa wasilipwe mishahara hadi watakapowasilisha vyeti husika.

“Tunakaribia kukamilisha uhakiki mwezi Septemba, hivyo tumeagiza kuwa watumishi wote wasiopeleka vyeti ili vihakikiwe wasilipwe mishahara hadi watakapopeleka vielelezo vyao,” Ndumbaro anakaaririwa.

Alisisitiza kuwa Serikali haitaongeza mishahara kwa watumishi wa umma hadi zoezi la kuhakiki vyeti feki litakapokamilika lakini malipo ya malimbikizo yasiyohusiana na mishahara yameshaanza kufanyika.

Katika hatua nyingine, Rais wa Tucta, Tumaini Nyamhokya aliwasilisha ombi la shirikisho hilo kwa serikali kuwa watumishi ambao walibainika kuwa na vyeti feki lakini wamebakiza mwaka mmoja kustaafu wafikiriwe kulipwa mafao yao.

Hata hivyo, Serikali imeendelea kushikilia msimamo uliotangazwa hivi karibuni na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angellah Kairuki kuwa hakutakuwa na mafao kwa mtumishi yoyote aliyeondolewa kwa vyeti feki.

Rais wa zamani wa Brazil ahukumiwa kwenda jela miaka tisa na nusu
McGregory atamba kumuaibisha Mayweather ndani ya raundi 4