Kufuatia hatua ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), kuruhusu vyombo vya habari, vyama vya siasa, mashirika ya kiraia na umma kwa ujumla kufanya majumuisho yao ya matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9, mambo yamekuwa ni tofauti na matarajio kutokana na takwimu zinazotofautiana.

Vyombo vya habari vimeanzisha vituo vyao vya kuhesabia kura kuhesabu matokeo ya uchaguzi wa urais, na wamekuwa wakitofautiana licha ya kuwa wote wanapata data kutoka kwa tume ya uchaguzi.

Hatua hiyo inaenda sambamba na uchakataji wa data wa wafanyakazi walio maeneo tofauti ambao bado haijafahamika ni kwanini wengi wao wamekuwa na namba ambazo zina taswira tofauti kiasi cha kuchanganya wafuatiliaji wa matokeo wanaoamini kuwa taarifa sahihi zitatolewa na vyombo vya Habari.

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini Kenya (IEBC), Wafula Chebukati.

IEBC, hupakia matokeo ya vituo vya kupigia kura, na vyombo vya habari huyapakua na kuyahesabu kisha kuiarifu jamii kupitia machapisho mbalimbali ya Habari ikiwemo mitandao ya kijamii.

Kwa kuzingatia uchapaji huo wa taarifa, hesabu za mashirika ya vyombo vya Habari huweka data kwa zilizochakatwa huku kukiwa hakuna hakikisho kwamba matokeo yote ni halali na ya mwisho kama yalivyotangazwa kwenye kituo cha kupigia kura.

Mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati mapema kabla ya uchaguzi alisema, “Kumbuka matokeo yanayotangazwa katika vituo vya kupigia kura ni ya mwisho na ndiyo yapo kwenye tovuti.”

Hata hivyo, matokeo ya tovuti ya umma ndiyo tume itayategemea wakati wa kujumlisha kura katika kituo cha kitaifa cha kuhesabia kura.

Kenya: Akaunti feki ya IEBC yafungwa
Simba SC yaomba radhi hadharani