Mahakama ya mapinduzi ya Iran imetoa hukumu ya kifo kwa watu watatu kwa kuhusika na machafuko yaliyotokea wakati wa maandamano ya kulalamikia kifo cha Mahsa Amini mikononi mwa polisi wa maadili.

Tovuti ya mahakama ya mapinduzi nchini Iran inayosikiliza kesi za masuala ya usalama imesema mshtakiwa wa kwanza ametiwa hatiani kwa kumgonga kwa gari lake na kumuua afisa wa Polisi wa pili kwa kumiliki bunduki na kumchoma kisu afisa wa usalama na wa tatu alitiwa hatiani kwa kuzuia magari barabarani na kueneza ugaidi.

Mkurugenzi wa shirika la kutetea haki za binadamu lenye makao yake nchini Norway IHR Mahmood Amiry-Moghaddam amelaani vikali hukumu hizo za kifo, na kutahadharisha juu ya uwezekano wa watu wengine kunyongwa. Iran hata hivyo inayashtumu mataifa ya Magharibi kwa kuchochea ghasia hizo.

Waandamanaji wakibeba picha ya Mahsa Amini

Shirika la ujasusi la Uingereza M16 limesema kuwa Iran inataka kuwateka nyara au kuwaua raia wa Uingereza ambao inawaona kama maadui wa serikali na kwamba matukio kama 10 ya njama dhidi ya raia hao yamefichuliwa.

Ghasia za mitaani ambazo zimeenea kote nchini humo zimezochochewa na kifo cha Mahsa Amini (22) mnamo Septemba 16, kijana huyo mwenye asili ya Kikurdi, alifariki akiwa chini ya ulinzi wa polisi wa maadili baada ya kukamatwa kwa madai ya kukiuka kanuni ya mavazi ya wanawake wa Iran.

Kwa mujibu wa video iliyochapishwa mtandaoni na mtandao maarufu unaofuatilia matukio ya siasa na maandamano nchini Iran wa 1500 Tasvir, waandamanaji walisikika wakiimbia kwenye barabara za mji mkuu Tehran “Tutapigana! Tutakufa! Tutaichukua Iran!”

Video nyengine iliyothibitishwa na shirika la habari la AFP, imeonyesha vikosi vya usalama, wakiwemo polisi waliovalia mavazi ya raia, wakiwashambulia wanawake wasiokuwa na vazi la hijabu kwenye treni ya chini ya ardhi.

Takriban watu saba wameripotiwa kupoteza maisha yao kufuatia ghasia hizo ndani ya muda wa siku mbili.

Mamlaka imekuwa ikizima mtandao wa intaneti na kufanya iwe vigumu kuthibitisha ripoti za ghasia zinazoripotiwa katika maeneo mengine ya Jamhuri hiyo ya Kiislamu.

Mbunge ajiuzulu sababu ya ulevi
Kenya yaondoa marufuku uagizaji GMO