Wataalam wa ndege wastaafu nchini wameishauri Serikali ya awamu ya Tano kuhakikisha inarudisha vitega uchumi muhimu vya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kwa kuwabana wote walioinyang’anya kampuni hiyo.

Mhandisi  mstaafu  wa shirika  la ndege la Taifa ATC,  J. Mwandimo ameiambia Dar24 kuwa ushauri huo ulitolewa katika kikao kilichofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na idadi kubwa ya wataalam wa ndege nchini.

Alisema wanampongeza Rais John Magufuli kwa kuisuka upya ATCL kwa kununua ndege za Bombardier Dash8-Q400 ambazo zinaendana na mazingira ya nchi pamoja na kuunda upya bodi ya kampuni hiyo lakini wanaamini ili ATCL irejee katika ubora wake ni lazima vitega uchumi vyote virudishwe mikononi mwake.

Aidha, mtaalam huyo alisema badala ya ATCL kutegemea kurusha ndege pekee kama chanzo muhimu cha mapato yake huku vitega uchumi vingine vikiwa mikononi mwa makampuni au mashirika binafsi kwa mfumo wa ubia, Serikali ihakikishe inaimiliki kampuni hiyo kwa asilimia 100 na kuipa nguvu ya kusimamia vitega uchumi vyote vya endeshaji wa ndege.

“ATCL ipewe uwezo wa kusimamia vitega uchumi katika viwanja (ground handling) ikiwa ni pamoja na kuipa mamlaka ATCL kutoa huduma zote muhimu kama kuhudumia abiria, kuhudumia mizigo yote ya ndege, kuhudumia vyakula ndani ya ndege na Lounge zote za first class (daraja la kwanza) pamoja na huduma za ‘booking za ndege,”  Mhandisi Mwandimo aliiambia Dar24.

Alisema kuwa wataalam hao pia walishauri kuundwa kwa kitengo maalum cha ATCL ambacho kitasimamia shughuli zote kwa kugawanywa katika maeneo ya usimamizi wa mizigo, abiria, mifumo ya kompyuta, mabasi ya kuwachukua abiria na mizigo, ulinzi na mengineyo.

Alisema walishauri pia Serikali kuunda na kukiwezesha ipasavyo kitengo cha uhandisi cha ATCL ambacho kinaweza kuwa chanzo cha kuzalisha mapato kwa kutengeneza ndege za kigeni pale zinapopata matatizo huku kikihakikishia uimara wa ndege za Serikali kwa gharama nafuu.

Mhandisi huyo alieleza kuwa kikao hicho pia kilipendekeza Serikali kuangalia namna ya kuipa ATCL uwezo wa kuuza mafuta ya ndege T3.

“Huduma ya kuuza  mafuta  ya ndege T3 sio lazima  apewe PUMA au Oil Com  kwa sababu biashara hii ina  maslahi  sana basi  serikali inaweza kuipa ATCL  ikishirikiana na kampuni  nyingine yenye uzoefu,” alisema.

Aliongeza kuwa kuiwezesha ATCL kutaisaidia Kampuni hiyo kujiendesha yenyewe na kuhimili ushindani wa soko ikiwa ni pamoja kuwalipa mishahara na stahiki zote wafanyakazi wake bila kutegemea kiasi chochote kutoka Wizara ya Fedha (Hazina).

“Tunarudia tena kumuomba Waziri wa Mawasiliano na uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amshauri Rais Magufuli kutumia mamlaka yake kurudisha vitega uchumi ambavyo ATCL iliporwa na Mafisadi waliokuwa katika Serikali za awamu ya pili, ya tatu na ya nne ambao hawakujali maslahi ya shirika la ndege la Taifa ATC/ATCL na badala yake wakayapa upendeleo mkubwa baadhi ya mashirika ya ndege ya mataifa mengine ambayo hayanufaishi nchi,” alisisitiza.

Alisema wahandisi hao walitahadharisha kuwa watakuwepo watu wengi wasiopenda maendeleo ya kampuni hiyo watakaopinga ushauri wao wakitaka ATCL ijikite katika biashara ya kurusha ndege tu.

“Tunaiomba serikali  ya awamu  ya tano  ihakikishe kuwa shirika  la ndege  la taifa ATCL linarudishiwa mamlaka ya kumiliki ground handling za airport zote  za tanzania bara  na hasa  viwanja vikubwa kama Julius Nyerere International Airport Dsm, Kilimanjaro International Air Port, Mwanza Air Port, Kigoma Air Port, Songwe Air Port, Mtwara Air Port, Dodoma Air Port n.k,” Dar24 inamkariri mhandisi Mwandimo.

Ushauri huo umekuja wakati ambapo Serikali imejikita katika kufufua na kuiwezesha ATCL kufanya biashara ya usafiri wa ndege nchini kwa gharama nafuu ambapo kesho Rais John Magufuli anatarajia kuzindua ndege mbili aina ya Bombardier Q400 zilizonunuliwa hivi karibuni.

TFF Yatangaza Viingilio Vya Mpambano Wa Young Africans Vs Simba
Majaliwa aiweka RUBADA kikaangoni, Asema inaendeshwa kwa ubabaishaji