Chama tawala nchini Nigeria kimepata pigo baada ya wabunge wake 15 kujiunga na chama kikuu cha upinzani ikiwa imebaki miezi michache kuelekea uchaguzi mkuu.

Taarifa iliyothibitishwa jana na kiongozi wa Seneti, Bukola Saraki imeeleza kuwa idadi hiyo ya wabunge imeondoka katika chama tawala cha All Progressives Congress (APC) na kujiunga na People’s Democratic Party (PDP).

Hatua hiyo ambayo ni pigo kubwa kwa Rais Muhammadu Buhari anayetarajia kuomba kuchaguliwa tena mwakani, imesababisha idadi ya wabunge wa chama tawala kuzidiwa na idadi ya wabunge wa chama hicho kikuu cha upinzani.

APC inakuwa na wabunge 49 huku PDP inakuwa na idadi ya wabunge 54, hali inayotishia maamuzi ya Serikali yatakapowekwa mezani ndani ya bunge hilo kujadiliwa na kupigiwa kura.

Msemaji wa APC, Bolaji Abdullahi alizungumza na waandishi wa habari kwa njia ya simu akiwa Abuja, ameeleza kuwa wamefanya jitihada za kuzuia hali hiyo lakini hawakufanikiwa.

“Kinachotokea sio kitu ambacho tumekiruhusu tu kitokee. Tumekuwa na majadiliano na wajumbe wetu hadi juzi usiku kuwashawishi wasiingie katika hatua hiyo,” alisema Abdullahi.

Buhari mwenye umri wa miaka 75, ambaye pia ni kiongozi wa zamani wa kijeshi, anatarajia kuwania muhula wa pili wa urais katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Februari mwakani. Buhari alifanikiwa kumshinda Rais aliyekuwa madarakani mwaka 2015 ikiwa ni mara ya kwanza katika historia ya nchi hiyo.

Gelson Martins asaini Atletico Madrid
Video: Chadema wajilipua, Polisi waliohusishwa mauaji ya Akwilina huru